Mchakato wa Kuandaa Kitabu cha Chimbuko, Muundo na Historia ya Ukoo wa Kivenule na Uhehe kwa Ujumla

Mchakato wa Kuandaa Kitabu cha Chimbuko, Muundo na Historia ya Ukoo wa Kivenule na Uhehe kwa Ujumla
Karibu uone yale ambayo KAUKI inafanya

Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI, 2014

Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI, 2014
Chimbuko na Muundo wa Ukoo wa Kivenule (2005 - 2009)

Mkutano Mkuu wa10 wa KAUKI

Mkutano Mkuu wa10 wa KAUKI
Tangazo la Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Wednesday 7 August 2013

TAARIFA YA UTENDAJI WA KAUKI MWAKA 2011 - 2012



Taarifa ya Utendaji wa KAUKI
Taarifa ya Utendaji wa KAUKI ya mwaka 2011/2012, ni mkusanyiko wa taarifa mbalimbali ambazo hukusanywa na viongozi Wakuu wa KAUKI na Viongozi wa Kanda kwa lengo la kuifahamisha jamii inayounda umoja huu, kutambua michakato mbalimbali ya maendeleo inayoendelea ndani na nje ya jamii hiyo. Taarifa ya utendaji hugusa maeneo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimaendeleo. Ni utaratibu wa KAUKI kutoa taarifa ya michakato mbalimbali ya maendeleo inayotokea Tanzania na hususani katika Kanda ambako matukio ya kila aina kuhusiana na maisha ya kila siku ya watu hutokea. Lengo lake kubwa ni kuwahabarisha wana-KAUKI kutambua mambo mbalimbali yaliyofanyika, hususani mipango ya maendeleo, mafanikio, matatizo na changamoto na namna walivyokabiliana na vizingiti mbalimbali kuelekea kupata mafanikio na maendeleo tarajiwa.

Taarifa ya Utendaji wa KAUKI imegawanyika katika sehemu kandaa kama inavyobainishwa hapa chini:

Maana ya KAUKI

KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka 2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi. Kuanzishwa kwa KAUKI kuliambatana na maandalizi yaliyojumuisha mikutano zaidi ya 10 ya mashauriano iliyofanyika sehemu mbalimbali Jijini Dar es Salaam na Kidamali, Iringa.

Dira ya KAUKI
Kuwa na jamii elewa, angavu na inayowajibika kwa kujitegemea.

Maono ya KAUKI
Kujengeana uwezo kwa kutumia raslimali, stadi, ujuzi, maarifa na weledi, kupitia mafunzo, kongamano, mijadala na mikutano ili kuboresha maisha.

Malengo ya KAUKI
Lengo Kuu
Kuinua na kuboresha maisha ya wanaukoo wa Kivenule, kielimu, kiuchumi na kisayansi kwa kutumia ujuzi, maarifa na raslimali zinazotunguka.

Malengo mengine mahsusi
1.   Kuujua, kuuelezea kiufasaa na kuchambua kwa mantiki Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule, pamoja koo mbalimbali za jamii za watu wanaoishi katika mkoa wa Iringa.
2.   Kuzikusanya, kuziratibu na kuzihifadhi taarifa na kumbukumbu mbalimbali za Ukoo wa Kivenule kutoka vyanzo rasmi na visivyo rasmi kwa nia ya kuielimisha jamii, kuhusiana na tabia na sifa ya kuzaliwa, kukua na kuenea kwa koo mbalimbali katika mkoa wa Iringa.
3.   Kuipa fursa Jamii inayounda KAUKI, kufahamiana na kutambuana, na pia kupeana fursa mbalimbali za kimaendeleo katika muktadha wa uchumi, siasa, utamaduni na siasa;
4.   Kufanya senza ya jamii inayounda KAUKI. Senza hiyo itajumuisha Wana-KAUKI waliohai na wafu. Lengo la mahususi la kufanya senza ni kupunguza kujirudia kwa majina kutokana na hatari zinazoweza kujitokea katika Mifumo ya Kompyuta (Database) ambayo hairuhusu majina kujirudia hususani katika mitihani, ajira na udahiri katika vyuo;
5.   Kuunzisha na Kuuboresha Mfuko wa KAUKI ili usaidie Kusomesha, Kutibu na Kutoa Msaada wa Dharura. Pia Mfuko wa KAUKI utasaidia kugharamia sehemu ya gharama za Mikutano Mikuu.
6.   Kuboresha Elimu ndani ya Ukoo wa Kivenule ili ndugu/wanaukoo wawe na uelewa wa hali juu na kumudu mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia katika Dunia ya Utandawazi;
7.   Kusuluhisha na kutatua matatizo yanayojitokeza katika Ukoo wa Kivenule kwa kupitia vikao vinavyokubalika;
8.   Kuelimisha Wanaukoo/ndugu kuhusiana na madhara ya ugonjwa wa UKIMWI, Malaria na matumizi ya Madawa ya Kulevya na Ulevi wa kupindukia;
9.   Kuinua na kuboresha  viwango vya maisha vya Wana-KAUKI ili waishi maisha mbadala yenye milo kamili, furaha na nyumba bora na nadhifu;
10.        Kuongeza na kuimarisha mahusiano mazuri ndani na nje ya ukoo kwa kushirikiana katika matatizo mfano raha, ugonjwa, misiba pamoja na majanga makubwa;
11.        Kuwa na nguvu ya kurekebisha tabia zisizostahili kwa wanaukoo/ndugu ndani ya Ukoo na kutafuta suluhu ya migogoro/migongano baina ya mtu au jamii inayotuzunguka;
12.        Wanaukoo kuutambua na kuuelewa mtawanyiko/mgawanyiko wa Ukoo wa Kivenule;
13.        Wanaukoo/ndugu kushirikiana katika shughuli za uzalishaji mali pamoja na utendaji kazi wa kila siku;
14.        Kushirikiana na umoja au vikundi vingine vilivyoungana ili kuuletea Ukoo wa Kivenule maendeleo endelevu;
15.        Kuanzisha Mfuko wa kukopeshana (SACOSS); na
16.        Kupunguza au kuondoa kabisa tabia ya uvivu na uzembe ndani ya Ukoo wa Kivenule.

Muundo wa KAUKI
KAUKI inaundwa na Kanda sita ambazo ni Kidamali, Irore, Nduli, Magubike, Mufindi na Dar eS Salaam. Kwa mujibu wa Katiba ya KAUKI, kuna Mkutano Mkuu ambao ndio mkutano mkubwa kuliko yote. Hufanyika mara moja kwa mwaka. Pia KAUKI ina mikutano ya Kamati ya Utendaji ambayo hufanyika mara nne kwa mwaka kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu. Katika Kanda pia kuna mikutano midogo midogo ambayo jukumu lake ni kujadili masuala yanayohusiana na maendeleo ya Kanda. Muundo wa Uongozi wa KAUKI upo kama ifuatavyo:

Uongozi Mkuu wa KAUKI
Uongozi mkuu wa KAUKI unaundwa na viongozi watano, kama inavyobainishwa hapa chini:
1.    Mwenyekiti:                   Donath P.  Mhapa
2.    Makamu Mwenyekiti:              Christian J. Kivenule
3.    Katibu:                          Adam A.    Kivenule
4.    Makamu Katibu:            
5.    Mweka Hazina                        Justin D.    Kivenule

Uongozi wa Kanda
Kila kanda ina kiongozi wake ambaye ni Mwenyekiti, ambaye naye husaidiana na Katibu. Pia ndani ya Kanda kuna viongozi wa Kamati mbalimbali ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba ya KAUKI. Kamati hizo ni:
1.    Kamati ya Mipango na Maendeleo;
2.    Kamati ya Mahesabu na Fedha;
3.    Kamati ya Nidhamu na Maadili; na
4.    Kamati ya Maafa na Matatizo.
Katiba ya KAUKI ndiyo mwongozi mkuu wa shughuli zote zinazofanywa na umoja huu. Katiba ya KAUKI ilipitishwa rasmi katika Mkutano MKuu wa Pili wa KAUKI uliofanyika Kidamali, Iringa.

Walezi wa KAUKI
KAUKI ilikuwa ina Walezi Watu ambao walichaguliwa kiujumla bila kuzingatia mgawanyo wa Kanda. Kutokana na matatizo mbalimbali ya usimamizi katika Kanda yanayotokana na kulegalega kwa usimamizi na utendaji wa viongozi katika kanda, na baada ya kuthmini shughuli za maendeleo ya KAUKI katika kanda, taarifa hii inashauri yafanyike maboresho kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa Walezi wa KAUKI. Maboresho hayo yafanyike kwa kuiwezesha kila Kanda kuwa na Mlezi wake, ambaye atapewa kazi na majukumu ya msingi. Majukumu hayo ni:
1.    Kuhamasisha Wana-KAUKI katika Kanda ili wawe na mwamko na hamasa katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya KAUKI. Kumekuwepo na kususua sua kwa shughuli za KAUKI katika Kanda hususani kushindwa kubisa kutekelezwa kwa shughuli za maendeleo, mfano kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, kushirikiana, kujumuika katika Mikutano Mikuu, utoaji wa michango ya kufanikisha Mikutano na Mfuko wa KAUKI. Kuwepo kwa Walezi katika Kanda kutasaidia katika kuwahimiza viongozi waliopewa majukumu kuwajibika kikamilifu, na pia kuishauri jamii inayounda KAUKI katika maeneo hayo, kujitoa kwa hali na mali ili kupata maendeleo.
2.    Kuwahimiza viongozi kuwajibika kwa mujibu wa nafasi zao. Majukumu yote ya viongozi yapo katika Katiba ya KAUKI. Hivyo pale ambapo itaonekana uongozi unazembea, Mlezi wa Kanda ana jukumu la kuwahimiza viongozi husika kujiwabika kwa mujibu wa majukumu yao ya kazi.

3.    Kuhudhuria vikao vyote vya Kanda ambavyo vitaitishwa na Viongozi wa Kanda wa KAUKI au vile vya Kamati mbalimbali za KAUKI katika Kanda, na Vikao vya Kamati vitakavyoitishwa na KAUKI.

4.    Kuitisha kikao/vikao katika Kanda kama kuna suala la msingi ambalo linapaswa kuzunguzwa na kujadiliwa kwa maendeleo ya KAUKI, na pia kama kutajitokeza suala la dharura au tatizo kwa mmoja wapo wa Wana-KAUKI kutoka katika Kanda husika.

Ukomo wa Uongozi kwa Viongozi wa KAUKI kwa mujibu wa Katiba, ni vipindi viwili vya miaka mitatu.

Historia Fupi ya Kuanzishwa kwa KAUKI
Harakati za kuanzishwa kwa KAUKI zilianza kwa kuratibu mawazo ya wana-ukoo wawili, yaani Ndugu Faustino Kivenule na Ndugu Christian Kivenule mwezi Desemba 2004. Mawazo hayo yalifanyiwa kazi kwa kumshirikisha pia Ndugu Adam Kivenule, ambaye bila kuchelewa, waliweza kuandaa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mashauriano, Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa River Side, tarehe 6 Februari, 2005 – Jijini Dar es Salaam.

Harakati nyingine za maandalizi zilielekezwa upande wa Kidamali, Irore na Nduli. Kwa upande wa Kidamali, Mkutano wa Kwanza wa Mashauriano kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulifanyika mwezi Mei ambapo wajumbe toka Dar es Salaam walisafiri kwenda huko ili kuwasilisha hoja, kufanya mashauriano na majadiliano, kuchagua viongozi wa kusimamia uratibu na kuunda kamati ya maandalizi.

Maeneo mengine kama Nduli na Irore hazikuweza kufanya maandalizi ya moja kwa moja japo taarifa toka Dar es Salaam ziliweza kufikishwa na baadhi ya wanaukoo wanaishi huko. Mjumbe mmoja tu ndugu Augustino Kivenule, toka Mgongo, Iringa ndiye aliyeweza kumudu kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule.

Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI
Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI ni mfululizo wa Mikutano Saba ambayo imekuwa ikifanyika toka mwaka 2005, ulipofanyika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa KAUKI. Takwimu zinaonesha kuwa mikutano mitatu imefanyika kijijini Kidamali na mkutano moja moja kufanyika Kijijini Irore, Nduli, Magubike na Igowole, Mufindi – Mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa makubaliano na utaratibu ambao umewekwa na Wana-KAUKI, mikutano hii itakuwa inafanyika katika ngazi ya Kanda, ili kuipa fursa jamii inayounda KAUKI kushiriki moja kwa moja. Lakini pia, vipaumbele huwekwa pale ambapo kuna idadi kubwa ya wana-KAUKI na Wana ari ya kuandaa mkutano kabla ya kuidhinishwa katika Mkutano Mkuu wa KAUKI. Japo hadi sasa, KAUKI Kwa msingi huo, Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI, kwa kauli moja, uliazimia kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI ufanyike katika Jiji la Dar es Salaam, tarehe 30 Juni – 01 Julai, 2012.

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI – Dar Es Salaam
Utaratibu umewekwa na Wana-KAUKI kuwajibika kufanya maandalizi ya hali na mali ili kuwezesha kufanikisha kufanyika kwa mikutano hii. Kama ilivyokwishafanyika katika mikutano iliyotangulia, utaratibu huo huo umeendelea kutumika katika kuandaa Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI. Pia  maandalizi mengine yamekuwa yakifanyika kwa ngazi ya Kanda, ambapo viongozi wa kanda husika wamebeba jukumu la kukusanya michango ya hali, fedha na nafaka ili isaidie katika kutoa huduma katika siku mbili za mkutano huu. Kanda zilizopaswa kushiriki katika mchakato wa maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI ni Kidamali, Magubike, Irore, Nduli na Mufindi. Hizi ni kanda ambazo katika mikutano mingi zimekuwa zikiwasilisha taarifa zake. Kila kanda inaelewa majukumu yake ambayo ni pamoja na kukusanya michango, kuhamasisha ushiriki wa wanandugu katika Mkutano wa Nane wa KAUKI Dar es Salaam na pia utoaji wa michango.

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI yalianza mapema tu mara baada kumalizika kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI. Maandalizi ya mkutano huu ni jukumu la kila mwana-ukoo ambapo atashiriki kwa kutoa mchango, nafaka, mfugo au nguvu zake katika kuhakikisha kuwa maandalizi ya mkutano yanaenda vizuri.
Katika Kanda ya Dar es Salaam, Katibu wa KAUKI kwa kushirikiana na Wana-KAUKI wanaoishi Dar es Salaam, walianza maandalizi mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI. Barua ifuatayo ilisambazwa kwa Wanaukoo wote wanaishi Dar es Salaam ili waweze kushauriana na kuweka mikakati namna ya kuweza kuandaa Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI.


Our Ref:
KAUKI./Ut./Kumb.I/030/11

Date:
Jumatatu, Julai 11, 2011
Your Ref:





________________________
________________________
________________________
________________________

Ndugu,

YAH: MWALIKO KATIKA MKUTANO WA KWANZA WA MASHAURIANO YA WANAUKOO
 WANAOISHI DAR ES SALAAM KUHUSU MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA
 NANE WA UMOJA WA UKOO WA KIVENULE (KAUKI)

Rejea kichwa cha habari hapo juu.

KAUKI ni Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ulioanzishwa rasmi mwaka 2005, kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, zinazoikabili jamii inayounda umoja huu; hususani katika kujikwamua na ugumu wa maisha na pia kutumia fursa zinazopatikana ili kukabiliana na kuondokana na wimbi la umaskini, ujinga, maradhi na utegemezi.

Dira ya KAUKI inajizatiti kuwa na jamii elewa, angavu na inayowajibika kwa kujitegemea; hali kadhalika Maono yake ikiwa ni kujengeana uwezo kwa kutumia raslimali, stadi, ujuzi, maarifa na weledi, kupitia mafunzo, kongamano, mijadala na mikutano ili kuboresha maisha.

Lengo kuu la KAUKI ni kuinua na kuboresha maisha ya wanaukoo, kielimu, kiuchumi na kisayansi kwa kutumia ujuzi, maarifa na raslimali zinazotuzunguka. Mipango ya KAUKI inajikita katika kujiimarisha katika ngazi zote za kiutendaji, kiuendeshaji na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, kisiasa, kimaendeleo na kimapinduzi.

Kwa muktadha huo, malengo mengine ya KAUKI ni pamoja na:
·         kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda zake;
·         kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa kusaidia wanaukoo katika elimu, afya na matatizo mengine. Tayari mfuko umeanzishwa na wanaukoo wanaombwa waendelee kuuchangia; 
·         Kumiliki sanduku la posta na tovuti. Tofuti yetu ya muda inapatikana kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com  na www.tagumtwa.blogoak.com  
·         Kufungua akaunti ya KAUKI benki. Akaunti tayari imefunguliwa na inajulikana kwa jina la: KAUKI, Benki ya NMB, Akaunti Namba 6052301709, Tawi la Mkwawa, Iringa Mjini;
·         kununua vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti;
·         kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake;
·         kubuni na kutekeleza miradi ambayo itawasadia wanajamii. Kwa mfano Irole wamebuni kuanzisha mradi wa kilimo cha Alizeti. Taarifa zaidi zilitolewa katika mkutano wa saba wa KAUKI;
·         Kuanzisha kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na ujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI kupitia maandiko ya miradi (project proposal and appraisal), pamoja na miradi mbalimbali ya ujasiamali. Suala hili lipo katika mchakato; na
·         Kuchapisha kitabu cha Historia ya Wahehe toleo la Kwanza: Ndani ya kitabu kutakuwa na sehemu zifuatazo: Historia ya Wahehe na Kuibuka kwa Tawala na Koo mbalimbali ndani ya Uhehe (Wanitole, Wahabeshi, Wangazija); Harakati za Mapambano ya Kikabila na Himaya mbalimbali (Vita za Luhota; Mkwawa na Wajerumani; Mkwawa na Mnyigumba; Mkwawa na Wabena, Wasangu na Himaya Mbalimbali; Sehemu ya Pili:  Historia ya Koo za Wahehe: Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule [Mtengelingoma Balama na akina Tagumtwa Kivenule], Vita za Vatawangu na Ushujaa wa Tagumtwa katika Vita; Sehemu ya Tatu: Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI); Mipango na Harakati zake katika kuwakwamua Wanaukoo katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi, kutoka zaidi ya Vijiji 25 vya Wilaya ya Iringa Vijijini;

Toka mwaka 2005 Mikutano ya KAUKI ilipoanza kufanyika, pamekuwepo na mwamko wa hali ya juu, ambapo wanaukoo wengi kutoka maeneo ya Iringa Vijijini na kwingineko wamekuwa wakihudhuria na kujifunza mambo muhimu ya kimaendeleo. Wastani wa washiriki 160 toka zaidi ya vijiji 20, wamekuwa wakihudhuria katika siku mbili za mikutano na kupata mafunzo mbalimbali kutokana na mada ambazo zimekuwa zikifundishwa. Hadi leo hii, tayari mikutano Saba ya KAUKI imekwisha fanyika. Takwimu zinaonesha kuwa mikutano mitatu imefanyika Kijijini Kidamali, na mkutano moja moja kijijini Irole, Nduli, Magubike-Iringa Vijijini na Igowole-Mufindi, mkoani Iringa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa yote yaliyoelezwa hapo juu, Kanda ya Dar es Salaam nayo kwa mara nyingine inapewa Jukumu la Kuandaa na Kuratibu Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI, uliopangwa kufanyika tarehe 30 Juni na Julai 01, 2012, Jijini Dar es Salaam. Uongozi wa KAUKI kwa kutambua umuhimu na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wanaukoo, hususani wewe, pamoja na wadau mbalimbali, katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo, umeamua kukushirikisha kikamilifu, katika suala hili, kuanzia katika hatua za awali za maandalizi. Wadau wanaoguswa na maandalizi ya mkutano huo ni pamoja na wewe mwenyewe, viongozi, pamoja na taasisi zenye mwelekeo wa kusaidia jitihada hizi. Kwa kutambua umuhimu wako na pia nafasi yako katika maendeleo ya jamii na ushiriki wako katika harakati mbalimbali za maendeleo; Uongozi wa KAUKI kwa heshima na taadhima, unakualika kuwa mmoja wa WASHIRIKI katika mkutano huo, utakaofanyika katika Ukumbi wa Chonya Inn, uliopo eneo la Ubungo River Side, Siku ya Jumapili ya tarehe ____ Agosti 2011, kuanzia saa 5:30 Asubuhi. Kufika kwako ndiyo mafanikio ya mkutano huo.

Agenda za mkutano zimeambatanishwa pamoja na barua hii.

Natanguliza shukrani zangu dhati,
  
   Wako katika kazi,




   Adam Kivenule
   Katibu - KAUKI

Hizi hapa chini nia miniti zilizochukuliwa kwenye kikao cha kwanza cha mashauriano kilichofanyika katika ukumbi wa Chonya Inn, Ubungo Riverside.

Kikao Cha Kwanza Cha KAUKI-Kanda Ya Dar Es Salaam Kuhusu Maandalizi Ya Mkutano Mkuu Wa Nane Wa Kauki

Agenda:
1.    Kufungua kikao
2.    Taarifa fupi kuhusu Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI uliofanyika Igowole, Mufindi, Iringa.
3.    Maazimio ya Mkutano Mkuu wa Saba
  • Kupanga Vipaumbele
  • Kubuni na kuanzisha miradi
  • Kushiriki vikao vya kamati ya utendaji
4.    Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI
5.    Mahali unapofanyika: Dar es Salaam
6.    Mkakati wa Maandalizi: 
  • Utekelezaji wa Miradi
  • Michango ya Mfuko: Ahadi kwa mwaka mzima
  • Michango ya mkutano: kupokea ahadi kwa kila mjumbe
  • Michango mingine
7.    Mahitaji/Vifaa Vinavyohitajika
  • Computer + Printer
  • Projekta (Projector)
  • TV set
  • Banners (Makutano Ubungo, Mwenge, Magomeni, Tazara na Kwenye eneo la Mkutano)
  • Kadi za Maombi ya Mchango
  • Name Tag kwa kila Mshiriki
  • Mabango [Posters and Cloths Banners]
  • Matangazo katika Redio
  • Coverage (TV, Radio, magazeti, press release, press conference)

UTANGULIZI
  • Historia fupi ya KAUKI
  • Dira
  • Maono
  • Lengo Kuu
  • Malengo Mengine
  • Mafanikio
  • Vipaumbele 2011 – 2011
  • Changamoto

MKUTANO MKUU WA 8 WA KAUKI
  • Mchakato wa maandalizi
  • Ushiriki
  • Michango
  • Mikakati
  • Changamoto

ORODHA YA NDUGU WA DAR
A.               KIVENULE
1.    Adam            Kivenule
2.    Onesmo        Kivenule
3.    Delfina          Kivenule
4.    Ignus            Kivenule
5.    Innocent               Kivenule
6.    Frank            Kivenule
7.    Flomina         Kivenule
8.    Monica          Kivenule
9.    Consolata              Kivenule
10.          Michelina           Kivenule
11.          Stuwart             Kivenule
12.          Brandino            Kivenule
13.          Priskus              Kivenule
14.          Magreth            Kivenule
15.          Vicky        Kivenule
16.          Delfinus             Kivenule
17.          Christian            Kivenule
18.          John          Kivenule
19.          Asia          Kivenule
20.          Christopher        Kivenule
21.          Peter         Kivenule
22.          Zubery              Kivenule
23.          Benadetha Kivenule
24.          Lucy         Kivenule
25.          Janeth               Kivenule
26.          Aneth                Kivenule
27.          Jachinda            Kivenule
28.          Raphael             Kivenule
29.          Lizeta                Kivenule
30.          Lugano              Sanga
31.          Maria                Kivenule
32.          Yasinta              Kivenule
33.          Mwamini            Kivenule
34.          Despina             Mhapa
35.          Athuman           Mtono
36.          Hamidu             Mtono
37.          Thabith              Mtono
38.          Zaina        Mtono
39.          Zaytuni             Mtono
40.          Nuhu         Mtono
41.          Mwanne            Mtono
42.          Zulfa         Mtono
43.          Sarah                Mapembe
44.          Evaristo             Mapembe
45.          Fredy                Mapembe
46.          Agnes               Mapembe
47.          Mzee         Mapembe

B.               Ndugu wengine kutoka IROLE, MAGUBIKE, KIDAMALI, NDULI, ITAGUTWA, MGONGO NA IGOMINYI, WANAOISHI DAR ES SALAAM
1.    Lemija          Mkini         Magubike
2.    Kulusumu              Mkini         Magubike
3.    Adam            Mnyavanu  Irole

MKAKATI WA MAKUSANYO YA MICHANGO
1.    Kuandaa CD yenye kuonesha Muundo WA Ukoo WA Kivenule, ambayo itasambazwa kwa watu ambao tutawaomba michango yao. CD hiyo itaambatanishwa na:
  • Kadi ya Kuomba Mchango wa Mkutano Mkuu wa Nane (8) wa KAUKI
  • Taarifa ya Jumla ya Utendaji wa KAUKI kwa kipindi cha Miaka Saba (7)
  • Ripoti ya Jumla ya KAUKI (2005 – 2011)
  • Barua ya Mwaliko wa Kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI.

2.    Kuandaa Miradi ambayo itasaidia kutunisha Mfuko wa KAUKI.
  • Miradi ya Kilimo cha Mahindi, Alizeti na Maharage
  • Kujiunga na Vikoba
  • Wana-KAUKI toka kanda husika kuahidi namna watakavyochangia Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI na pia kuboresha Mfuko wa KAUKI, mbali ya Mchango wa Kila wa shilingi Mia Tano (500/-) na Elfu Moja (1,000/-) kwa mwezi.

3.    Kuomba Ufadhili toka kwa Makampuni mbalimbali mfano VODACom, Airtel, Tigo, Zantel na Serengeti Lager. Makampuni hayo yanaweza kusaidia:
  • Kuandaa Mabango (Posters)
  • Kuandaa Tshirts na Caps
  • Kuandaa Banners
  • Wanaukoo kuchangia Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI kwa kutuma ujumbe mfupi katika simu zao kwenda mtandao uliojiunga nao.    

KALENDA YA VIKAO VYA KAUKI KANDA YA DAR ES SALAAM
·         JULY 2011: Kuandaa barua na nyaraka mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa kuanza maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI. Hii ni pamoja na kuandaa barua, kuandaa kalenda ya vikao na pia kutambua ndugu mbalimbali ambao wanaishi katika jiji la Dar es Salaam ambao jukumu lao litakuwa ni kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mkutano huo kupitia mlolongo wa vikao vingi ambavyo vitakuwa vinaitishwa kila mwezi. Na la mwisho ni kuandaa ajenda kwa ajili ya kikao kitakachofanyika mwezi wa nane.
·         AGOSTI 2011: Kupata taarifa ya Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI, uliofanyika Igowole, Mufindi – Iringa. Lengo ni kupanga mikakati ya utekelezaji ya masuala muhimu ambayo yatasaidia kufanikisha Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI, ambao utafanyika jijini Dar es Salaam.
·         SEPTEMBA 2011: Mwendelezo wa utekelezaji wa  yale ambayo tumekubaliana katika kikao cha mwezi Agosti 2010. Pia kutakuwa na kikao ambacho kitafanyika kwa lengo la kujadili yale ambayo tumekubaliana yawe sehemu ya utekelezaji. Pia kuanza kukusanya michango.
·         OKTOBA 2011
·         NOVEMBA 2011
·         DESEMBA 2011
·         JANUARI 2012
·         FEBRUARI 2012
·         MACHI 2012
·         APRILI 2012
·         MEI 2012
·         JUNI 2012

Kifupi, tulianza vizuri kwa kujiwekea mpango kazi mkakati katika kipindi cha mwezi Agosti, Septemba na Oktoba mwaka jana. Kwa bahati mbaya, mahudhurio yakabadilika na kuwa mabaya na hivyo kushindwa kuendelea kutekeleza mkakati wetu. Ndio maana baadhi ya miezi hatujaweza kubainisha chochote.

URATIBU WA SHUGHULI ZA KAUKI NA MIKUTANO
Shughuli za KAUKI zinafanyika chini ya mwongozo ambao ni Katiba ya Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI). Katiba hii ilishaanza kutumika mara tu baada ya Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI uliofanyika tarehe 24 na 25 Juni 2006. Nakala kadhaa za KAUKI tayari zimetolewa, kusambazwa na zinaendelea kutumika.

Kwa mujibu wa Katiba ya KAUKI, kuna viongozi mbalimbali ambao huchaguliwa kila baada ya kipindi cha miaka mitatu. Kuna viongozi wakuu wa KAUKI na Viongozi wa Kanda. Kila kanda ina kiongozi zaidi ya mmoja. Viongozi hawa, wanawajibika kwa wanaukoo wanaotoka katika Kanda husika.

Wajibu wa viongozi hawa, ni kushirikiana pamoja na Viongozi wa KAUKI katika kutekeleza masuala mbalimbali ya maendeleo yanayouhusu wana-KAUKI. Pia, ni wajibu wa viongozi hawa, kuwashauri Viongozi wa KAUKI katika masuala mbambali yanayoukabili ukoo wetu kwa mfano masuala ya ugonjwa, elimu, uchumi na maendeleo.

Viongozi wa Kanda wana nguvu ya Kikatiba katika kutimiza wajibu wao na pia wana wajibu wa kuhakikisha kuwa mipango mbalimbali inayopangwa kupitia Kamati Kuu au Mkutano Mkuu wa KAUKI inatekelezwa.

Viongozi wa ngazi nyingine za juu kama Katibu, Mwenyekiti, Makamu wa Katibu, Makamu wa Mwenyekiti, Mweka Hazina na Msaidizi wake, wana wajibu wa kuwahimiza viongozi wa Kanda, kushirikiana baina yao wenyewe na pia kushirikiana na viongozi wakuu kutekeleza wajibu na majukumu mbalimbali ambayo yanatukabili.

Kwa mujibu wa KAUKI, viongozi wa Kanda, wana wajibu kuhudhuria vikao mbalimbali kama inavyoainishwa kwenye Katiba ya KAUKI. Wajibu huo pia unawagusa viongozi wengine wa KAUKI na wanawajibika ipasavyo kutekeleza na kutimiza wajibu wao.

MICHANGO YA MFUKO WA KAUKI

Kama ilivyokubaliwa kwenye Mkutano Mkuu wa Pili wa KAUKI; na kama Katiba ya KAUKI inavyoainisha katika Ibara ya 5:3(ii), kuhusiana na wajibu wa kila mwanaukoo, kuwa kila mwanaukoo, anawajibika kulipa michango na kuchangia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa KAUKI kama atakavyoelekezwa na uongozi. Katiba ya KAUKI inafafanua kwa mapana kuhusiana na michango mbalimbali hususani michango ya kila mwezi. Katiba ya KAUKI, inaeleza wazi Matumizi ya michango hiyo ni kuwasaidia wanaukoo katika matatizo mbalimbali ya ugonjwa, masomo na pia kiuchumi pindi mfuko huo utakuwa umetuna, na kama kila mwanaukoo kuuchangia kikamilifu. Pia michango hiyo itasaidia gharama mbalimbali mfano kufanya mikutano.

Viongozi wa Kanda, walipewa jukumu la kukusanya michango hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa KAUKI, stakabadhi zikiwa na mhuri wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI), zilisambazwa kwa viongozi husika wa Kanda kwa ajili ya shughuli za ukusanyaji wa michango hiyo. Kila anayetoa mchango ni lazima apewe stakabadhi ya malipo halali na si vinginevyo.

Lakini viwango hivi vinavyotajwa kwenye Katiba havimfungi mwanaukoo kutoa zaidi. Mara nyingi katika utoaji wa michango kwa ajili ya maandalizi ya Mikutano Mikuu, kadi huandaliwa na kusambazwa kwa wana ndugu mbalimbali na pia kwa jamaa na marafiki zetu. Jambo hili ni nzuri kwa sababu linaonyesha heshima kwa yule unayemwomba atoe mchango wako. Kwa sababu hiyo, kadi maalum huandaliwa na kila mmoja wetu ambaye anahitaji kadi hupewa kwa kiwango kile kinachotakiwa.

Pia, viongozi wa KAUKI walipendekeza wanaukoo kuwa wabunifu katika kutoa michango yao, hii ni pamoja na kutoa bidhaa au mazao ambayo yatajulikana kama mchango. Kama ni nafaka au mifugo, inaweza kutumika kama chakula moja kwa moja au ikauzwa na zikapatikana fedha ambazo zitajumuishwa kwenye bajeti inayoandaliwa.

MICHANGO TOKA VYANZO VINGINE

Vipaumbele viliwekwa hususani katika kubuni miradi ambayo inaweza kusaidia kuboreshea mapato ya KAUKI na pia ya kila mwana-KAUKI. Licha ya kuwa ni kazi ya kamati ya mipango ya maendeleo, katika Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI, vipaumbele viliwekwa ili kuboresha kuboresha Mfuko wa KAUKI na pia kuboresha huduma katika Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI wa 2011 – 2012. Vipaumbele hivyo vilikuwa ni kuanzisha miradiya maendeleo katika kanda kulingana na mazingira  ya eneo husika. Lazima wana-KAUKI katika kanda zao, kuwa wabunifu wa shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Mfano, tunaweza kubuni miradi ya maandazi, chapati, mama lishe, kilimo au miradi yoyote ambayo mnadhani itatusadia kupata fedha kwa ajili ya kuweza kufanikisha mikutano kama hii na kutunisha Mfuko.

TAREHE YA MKUTANO MKUU WA NANE WA KAUKI

Mkutano Mkuu wa Sita wa KAUKI kwa kauli moja uliazimia Mkutano wa Saba wa KAUKI, ufanyike tarehe 30 Juni ya Jumamosi na 01 ya Julai Jumapili ya mwaka 2012, Jijini Dar es Salaam.

YALIYOJIRI KATIKA MKUTANO MKUU WA SABA WA KAUKI

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano, kutakuwa na shughuli mbalimbali katika siku mbili za mkutano. Pamoja na mambo mengine, kutakuwepo na uwasilisha wa mada kadhaa na pia taarifa mbalimbali kutoka kwa wana-KAUKI na viongozi, mfano:
·         Mada:   1.CHIMBUKO NA HISTORIA YA UKOO WA KIVENULE
2. CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI KAUKI KUJILETEA MAENDELEO
3. HISTORIA YA WAHEHE
·         TAARIFA YA UTENDAJI WA KAUKI
·         TAARIFA YA SHUGHULI ZA MAENDELEO KATIKA KANDA
·         KUSOMA RIPOTI YA MKUTANO MKUU WA TANO WA KAUKI
·         UZOEFU WA WANAUKOO KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO
·         MAJADILIANO YA HOJA MBALIMBALI AMBAZO ZIMEWASILISHWA NA WASHIRIKI KATIKA MKUTANO
·         MAHITAJI YA KAUKI NA JINSI YA KUFANIKISHA KUPATIKANA KWA MAHITAJI HAYO: Huu ni mjadala wa jumla na kila mjumbe wa mkutano anashiriki moja kwa moja kutoa mawazo yake. Katibu na watendaji wengine wa KAUKI wana jukumu ya kuyanakili maswali na majibu yote kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
·         MAJUMUISHO NA TATHMINI YA MKUTANO
·         MIPANGO NA MIKAKATI YA MBELENI
·         KUTANGAZWA KWA TAREHE YA MKUTANO MKUU WA SABA
·         SHUKRANI
·         KUFUNGA MKUTANO

UTAMBULISHO NA KUBALISHANA MAWAZO
Utambulisho baina ya wanaukoo utafanyika kwa kina na kila ndugu/mwanaukoo kuwa na kitambulisho ambacho alikivaa kifuani kwake. Kulikuwa na fursa mbalimbali kwa wanandugu kupeana uzoefu mbalimbali wa utafutaji wa maisha bora. Mbinu za kujiinua kimaisha zitafundishwa na wadau wenye uzoefu pamoja na aina mbalimbali za miradi ambayo ndugu wanaweza kufanya.

Kulikuwa na kipindi cha kupeana uzoefu wa shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka katika maeneo mbalimbali ambako ndugu wanaishi. Kama ilivyofanyika katika Mikutano Mikuu ya KAUKI iliyotangulia, maeneo yatakayotolewa uzoefu Kilimo, biashara na ajira kutoka katika maeneo mbalimbali. Kwa kupeana elimu ya ujasiliamali itasaidia kutufungua macho na hivyo kuongeza uwezo wa kufikiri na kwenda kutafuta maisha katika maeneo ambayo ni mbadala kwetu. Pia taarifa hizi zitawasaidia wanandugu toka maeneo mengine kupata mwanga wa shughuli mbadala zitakazosaidia kupata kipato na kuboresha maisha.

Angalizo: Viongozi wa Kamati ya Mahesabu na Fedha, watashirikiana na Mweka Hazina katika kuratibu shughuli zote za ukusanyaji wa michango mbalimbali, wakati wa maafa, wakati wa mkutano mkuu, mikutano na pia mchango wa kila mwezi.

MIPANGO YA KAUKI

KAUKI inajikita kujiimarisha katika ngazi zote za kiutendaji, kiuendeshaji na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, kisiasa, kimaendeleo, na kimapinduzi. Na kwa mujibu wa Mkutano wa Saba wa KAUKI, kulikuwa na mkakati wa kutekeleza vipaumbele ambavyo tulijiwekea kama KAUKI. Lakini, baadhi ya mikakati ya muda mrefu ya KAUKI ni pamoja na:
1.   KAUKI kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda ambapo wanaukoo wanadhani ni muhimu kuwa na ofisi. Jambo hili lilishaanza kufanyiwa kazi na pia eneo ambalo inabidi ofisi iwepo lilishapatikana katika majadiliano ya awali ya mwaka 2008. Viongozi toka eneo ambalo ofisi inabidi ifunguliwe watatuhabarisha zaidi wapi wamefikia.
2.   Suala na pili ni kupata usajili ili tuwe na fursa ya kufanya shughuli kubwa zaidi. Bado suala hili lipo katika mchakato, na taratibu nyingine zote za namna ya kupata usajili zilikwisha fuatiliwa. Ni matumaini yetu uongozi mpya uliochaguliwa, unalifanyia kazi kazi jukumu hili muhimu.
3.   KAUKI kuwa na sanduku lake la posta. Bado jambo hili halijatekelezwa na natumaini hatua za makusudi inabidi zichukuliwe. Hakuna masharti makubwa zaidi ya kulipa fedha tu. Ni changamoto kwa viongozi wa KAUKI na nadhani hatuna haja ya kusubiri zaidi ya kuchukua hatua zinazostahili kulikamilisha hili.
4.   Kuwa na Akaunti katika Benki yeyote. Ufunguzi wa Akaunti ulikwisha fanyika kabla ya Mkutano Mkuu wa Nne wa KAUKI uliofanyika Irole. Hima wanaukoo tutoe michango yetu na pia tusaidie kuitunisha akaunti yetu. Wangapi wanalipa mia tano za kila mwezi? Mnapata stakabadhi? Wangapi bado hawajalipa? Kwa nini? Hizi ndizo changamoto kwetu. Bila kujitoa hatuwezi kufanikiwa. Msitegemea watu wachache tu ndio wanaoweza kubadili maisha ya wanaukoo wote. Inabidi tuunganishe nguvu zetu wote. Wahenga walisema, ‘Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’.
5.   KAUKI kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti. Bado kutekelezwa kutokana na uhaba wa fedha na pia bado wanaukoo hawajaonesha mwito wa kutoa michango ya kila mwezi. Hivyo tunawahimiza kutoa michango hiyo ili baadhi ya mipango na malengo ya KAUKI yakamilike. Tutafanya harambee ili tuweze kununua vifaa hivyo, mfano Kompyuta na printa yake. Wangapi mpo tayari kuchangia?
6.   KAUKI kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Tumeanza na sehemu ndogo na mojawapo ni wakati wa mikutano hii. Lakini bado tunadhani inabidi tutafute fursa nyingine. Kama tungekamilisha suala la ofisi, natumaini fursa nyingi za kupata masomo kwa wana-ukoo zingetafutwa kwa hali na mali.
7.   KAUKI kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ambayo itawasadia wanajamii. Sijapata taarifa rasmi labda viongozi wa Irole wanaweza kutupa taarifa. Mwenyekiti wa kipindi kilichopita Bwana Nyakunga aliahidi kuwa wangeanzisha mradi wa alizeti, Sijui walifikia wapi? Tupatieni taarifa. Tuanzishe mashamba ya KAUKI na kila kanda iwe na shamba lake. Mazao yatakayopatikana yatatumika kama sehemu ya chakula wakati wa mikutano hii. Na pia iliyobaki itauzwa na fedha kuwekwa katika mfuko wa KAUKI.
8.   KAUKI kuwa na kitengo cha Utaalam wa Kitaaluma na Kiujuzi ambacho kitafanya shughuli za kuiletea fedha KAUKI, pamoja na miradi mbalimbali. Tunasubiri kukamilika kwa ofisi na kazi itaanza mara moja. Binafsi nipo tayari kujitolea kuhakikisha tunafanikiwa katika suala hili.
9.   KAUKI kujitangaza kwa asasi nyingine za ndani ya nchi na nje kwa kutumia teknolojia ya kisasa yaani kuwa na tovuti. Tumeanzisha tovuti (blog) na natumaini bado haijafikiwa na wengi. Mpango mzuri ni sisi wenyewe kulisajili jina la KAUKI (Domain Registration) kwa wamiliki wa mitandao na kuiweka hewani tovuti yetu kwa watoa huduma za mawasiliano ya tovuti na mitandao.
10.        Kuchapisha kitabu toleo la kwanza cha Umoja wa Ukoo wa Kivenule kwa kipindi cha mwaka 2008 – 2009. Kamati iliyoundwa imeshindwa kukutana na kuikamilisha kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za:
§        Kukosa pesa
§        Mtawanyiko wa wajumbe
§        Shughuli yenyewe inahitaji pesa kwa mfano kazi ya uhariri na uchapishaji
Kutokana shughuli kuwa ngumu na kushindwa kufanyika kama ilivyopangwa, inabidi kamati iwasilishe taarifa na mapendekezo kwa wajumbe kuhusu hatua ambazo imechukua na nini imekifanya; na pia nini kifanyike, kwa kurejea hadidu zake na pia majukumu yaliyopaswa kufanyika kabla ya mkutano huu wa tano.

MAPUNGUFU YA KAUKI NA WATENDAJI WAKE
Uongozi wa KAUKI bado umeonyesha mapungufu na hii pia inaathiri mfumo mzima wa utendaji kazi zake. Baadhi ya mapungufu hayo ni pamoja na kushindwa kubisa kutekeleza baadhi ya mikakati ambayo ilikuwa ni sehemu ya makubaliano na pia mipango ya mbeleni ya maendeleo ya KAUKI. Kwa mfano baadhi ya majukumu ambayo bado hayajatekelezwa ni pamoja na:-
1.   Kutotekelezwa kwa shughuli zilizo katika Kalenda ya Shughuli za Mwaka;
2.   Kushindwa kufanya vikao vya Kamati Kuu;
3.   Ushirikiano finyu baina ya viongozi wa ngazi mbalimbali wa KAUKI kutokuwepo kwa mpango-kazi, tathmini ya utendaji kazi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo;
4.   Viongozi wengi wa KAUKI kushindwa kutekeleza wajibu wao;
5.   Makusanyo hafifu ya michango; Wangapi wamelipa mpaka muda huu?
6.   Viongozi kutokuwa mfano mzuri katika kutoa michango. Tunaamini kiongozi lazima awe ni mfano wa kuigwa; Je viongozi wote mnatoa michango ya kila mwezi. Wangapi wamelipa mpaka muda huu?
7.   Wanaukoo kuonesha mwitikio duni katika ushiriki wa Mikutano Mikuu. Mfano wa Wanaukoo kutoka Dar es Salaam; na
8.   KAUKI kutokuwa na ofisi katika Kanda. Hii ni changamoto kwa viongozi wetu.

Taarifa za Maendeleo katika Kanda
Taarifa kwa Ujumla
Kwa wastani taarifa za Maendeleo katika Kanda hazidhirishi sana ukilinganisha na jitihadi ambazo zimefanywa na KAUKI kwa kipindi cha miaka saba ya uhai wake, kutekeleza majukumu yake na kuimarisha, kuoboresha na kuchagiza maendeleo katika nyanja zote, ushirikiano na mahusiano baina ya jamii. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi kanda, kumekuwepo na kusuasua kwa ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo katika jamii, hususani kushiriki katika kuinua elimu, kuboresha michango ya Mfuko wa KAUKI, kujitolea katika maandalizi ya Mikutano Mikuu ya KAUKI, na hata katika furaha na shida.

Mfuko wa KAUKI umekuwa ukichangiwa na watu wachache kabisa tofauti na kusudio la awali, ambalo pia kwa upande mwingine lingesaidia kuboresha mapato ya mfuko na hivyo kuanza kuisadia jamii inayounda umoja huo. Licha ya kupangia kiwango kidogo cha shilingi mia tano, bado mwenendo wa makusanyo ya mwaka ni duni kabisa ukilinganisha na idadi ya jamii inayounda KAUKI katika Kanda.

Makusanyo kiduchu ya michango yanachelewesha kuanza kutumika kwa fedha za mfuko kwa sababu kiasi kilichokusanywa bado ni kidogo sana. Wakati sasa umefika kwa Wana-KAUKI kuwa na vipaumbele ambavyo vitasaidia kuboresha mfuko wa KAUKI. Kabla ilivyopendekezwa katika Mikutano Mikuu ya KAUKI iliyopita, ambapo suala la uanzishaji miradi ambayo itaongeza tija na kuboresha mifuko, ni bora ukazingatiwa zaidi, hasa baada ya kufanya tathmini ya makusanya kwa kipindi cha miaka mitano.

Zoezi la kufanya sensa ya wana-KAUKI nalo bado limeendelea kusuasua katika kanda zote, licha ya msisitizo ambao ulikuwa umewekwa wa kuhakikisha kuwa, zinakusanywa taarifa mbalimbali za jamii inayounda KAUKI.

Changamoto za KAUKI Kanda ya Dar eS Salaam
KAUKI kanda ya Dar es Salaam imekutana na changamoto nyingi katika mchakato mzima wa maendeleo ya KAUKI. Mwitikio duni na pia kutokuwepo kwa ushirikiano kwa baadhi ya Wana-KAUKI imekuwa ni changamoto kubwa. Licha ya kuwepo mfumo wa kupeana taarifa kwa ujumbe wa simu wakati wa kuitana kwenye vikao, hali imekuwa tofauti. Kuna baadhi ya Wana-KAUKi ambao walidiriki kuhudhuria kikao kimoja au viwali vya awali na kupotea jumla. Wana-KAUKI wengine wamediriki kudanganya, hasa wakati tukiwajulisha kuja kwenye vikao vya maandalizi. Nanukuu, ‘nitakuja bila kukosa na kuleta mchango’, mwisho wa yote, hakuna mtu anayeonekana.

Kwa tathmini fupi, Wana-KAUKI toka kanda ya Irole wameonesha mwitikio duni. Kuna baadhi ambao wamekuwa wakiitikia mara zote na hawazidi watatu. Tumeendelea kusisitiza katika vikao vyetu, hata kama huna mchango ni vyema ukaja tukashirikiana. Lengo letu ni kuimarisha umoja. Tuna mengi ya kujifunza kutokana na hali hii.

Pamoja na kuwa KAUKI sasa ina umri wa miaka 8, binafsi kama kiongozi ambaye nimekuwa katika harakati hizi kwa kipindi kirefu, nakatishwa tamaa. Pengine uongozi ambao umekuwa ukifanya kazi kwa kipindi hicho umeshindwa kuonesha dira na pia kuwepo kwa hamasa ndogo na ufahamu finyi wa Wana-KAUKI juu ya malengo ya KAUKI pengine unachangia kusuasua kwake.

Katika Mkutano Mkuu wa Nane, katika kipengele cha Changamoto zinazoikabili KAUKI, inabidi mjadala mkubwa uegemee kwenye suala nzima la hamasa na mwitikio duni wa Wana-KAUKI katika umoja wetu.

Kwa mfano makusanyo ya michango ya KAUKi hayajaridhisha kabisa, licha ya taarifa za Mkutano huu kuanza kusambazwa toka mwezi Julai na Agosti mwaka 2011. Tulifanya maandalizi ya mapema ili angalau Wana-KAUKi wapate fursa ya kuchangia kidogo kidogo, lakini wengi wao hawakuweza kuona umuhimu wa hili. Wamekaa kimya kipindi chote cha mwaka na katika hatua za mwisho, kila mmoja anatoa sababu za hali ngumu. Hatukatai kuhusu ugumu wa maisha na hali mbaya ya uchumi. Tuliwaeleza hata kama huna uwezo wa kutoa mchango kufikia kile kiwango ambacho tulijiwekea, angalau wajaribu kutoa kidogo walichonacho. Nadhani, katika vikundi tutapata fursa ya kuzijadili changamoto hizi.

TANZIA
Uongozi wa KAUKI kwa niaba ya jamii nzima inayounda umoja huu, inatoa masikitiko yake kutoka na kifo cha Marehemu Xavery Sigatambule Kivenule, kilichotokea siku ya Jumatatu ya tarehe 22 Machi 2012, katika hospitali ya Mafinga, Iringa.

Ni hali ya kusikitisha kwa sababu mchango wake katika maendeleo ya KAUKI ulikuwa ni mkubwa. Kabla ya mauti kumfika, Ndugu Xavery Kivenule aliandaa na kufanikisha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI, uliofanyika Kijijini Igowole, Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa. Licha ya kuwa wachache walimudu kufanikisha mkutano huo ambao ulifanyika kama kawaida na kufanikiwa.

Ikumbukwe kuwa, Mkutano Mkuu wa Saba wa KAUKI ndio uliotoa maazimio ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI mkoani Dar eS Salaam. Wajumbe walioshiriki mkutano huo kwa Kauli  Moja, waliafikiana na Kukubaliana kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa KAUKI, ufanyika Jijini Dar es Salaam, tarehe 31 ya Juni na tarehe 01 ya Julai, 2012.

Mazishi ya Marehemu Xavery Sigatambule Kivenule yalifanyika Kijijini Igowole, Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa mnamo saa 6.00 ya tarehe 23 Machi 2012.

Marehemu Xavery Sigatambule Kivenule ataendelea kukumbukwa na Wana-KAUKI kwa mchango na hamasa yake katika kuhakikisha kuwa umoja huu unaendelea na kufanikiwa katika uhai wake.

Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi, Amina.


Kwa taarifa na mawasiliano unaweza kutufikia kupitia.

Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI)
Kando ya Barabara ya Hifadhi ya Ruaha
Sanduku la Posta 193
Kidamali, Iringa
Simu: +255 713 270364 (Katibu Mkuu-KAUKI)
Barua-pepe:        kauki2006@gmail.com
                            kivenule@gmail.com
                            tagumtwa.kauki@gmail.com
Blogu:        http://www.kauki-kauki.blogspot.com
                  http://www.tagumtwa.blogoak.com
                  http://www.tagumtwafoundation.wetpaint.com

Twitter:      https://twitter.com/kivenule
Facebook: https://www.facebook.com/kivenule
 



No comments:

Post a Comment