AGIZO LA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI KWA JESHI LA
POLISI NA SUMATRA KUFANYA UKAGUZI WA KINA KWENYE VYOMBO VYA USAFIRISHAJI KABLA
YA KUPEWA LESENI ITAKUWA NI KIINI MACHO
Katika maisha
yetu ya kila siku, kuna misemo mbalimbali ambayo hupenda kuitumia kama
miongozo, msisitizo, onyo na pengine kejeli kwa jamii husika. Kwa mfano, kuna
methali inayosema, 'Kawaida ni Kama Sheria', 'Kamba Hukatika Pembemba, 'Kukunjua
Makucha', 'Mwenye Macho Haambiwi Tazama'. Kila mmoja wapo ya msemo huu, una
maana ndani yake.Labda kidogo tu niegemee kwenye msemo huu, 'Kawaida ni Kama
Sheria', natumai kila mmoja wetu au wachambuzi wa masuala ya lugha wanaweza
kutoa tafsiri zao kulingana na upeo na uzoefu wao wa kila siku katika uchambuzi
wa lugha. Msemo huu, upo wazi kabisa. Kwa maana kuwa, kuna mambo ambayo
yanafanyika mara kwa mara katika jamii yetu. Kutokana na kufanyika huko, basi
jamii huamua kuhalalisha na kuwa mambo ya kawaida.
Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani Ndugu Pereira Ame Silima, si mgeni hapa Tanzania. Natumaini kuwa
unaufahamu vizuri msemo huu. Suala la tatizo la rushwa kwa jeshi la polisi hususani katika kitengo cha
Trafiki ni jambo la kawaida. Lakini, Bwana Silima atambue kuwa, Tanzania
inanuka rushwa ya hali ya juu. Takwimu za the East Africa Bribery Index (EABI)
ya mwaka 2011, Tanzania ilishika nafasi ya 3 kwa kiwango cha juu cha rushwa,
katika eneo la Afrika Mashariki, huku Burundi ikiwa ya Kwanza, na Uganda ya
Pili. Hali kadhalika Jeshi la Polisi katika nchi zote za Afrika Mashariki,
lilishika nafasi ya Kwanza. Kwa kifupi, unaweza kuona namna rushwa
ilivyoshamiri katika jeshi la polisi.
Kuna msemo mwingine ambao umeenea katika jamii yetu, ambao unasema kuwa,
Mpe Mchawi Akulelee Mwana (Mtoto). Hii ina maanisha kuwa, kwa sababu mtu mchawi
ana tabia ya kuua watu, ukimpatia mtoto akulelee hawezi kumwua. Hali ni tofauti
katika Jeshi la Polisi na hasa kitengo cha Trafiki, licha ya kubainika wazi
kuwa wamekithiri kwa vitendo vya rushwa, na wanaipokea kila siku, bado
watendaji hawa wa serikali, kama Naibu Waziri, wanarikirimu mamlaka na madaraka
makubwa kama ya kufanya ukaguzi kwenye vyombo vya usafiri ili viweze kupatiwa
leseni. Hii ni sawa na kumweka mbuzi mdomoni mwa Simba. Ule msemo wa 'mpe
mchawi akulelee mwana', haupaswa kutumika kwa Jeshi la Polisi, hususani kitengo
cha Trafiki, kwenye suala muhimu kama hili la kufanya ukaguzi ili leseni za
usafirishaji zitolewe. Hapa, hata ukimpa mchawi mtoto akulelee, atamwua tu.
Waziri atambue kuwa misemo nayo inaenda kwa wakati. Huu si wakati wake tena
kuutumia msemo huu.
SUMATRA kama wanavyojiita kuwa ndio wenye mamlaka ya kudhibiti vyombo vya
usafiri nchi kavu na majini, hawana tofauti na Trafiki. Mfano mdogo tu ni kuzama
mfululizo kwa boti za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar na kutoka Zanzibar
kwenda Pemba (MV Spice Islander na MV Skagit). Ndani ya miezi 10, zaidi abiria
mia tatu (300) idadi iliyotolewa na serikali, waliweza kupoteza maisha, huku
takwimu halisi za abiria waliopenda katika vyombo hivyo vya majini wakishindwa
kujulikana. Hakuna hatu mtu mmoja ambaye ameweza kuwajibika au kuwajibishwa na
mamlaka husika. Kuzama kwa Meli hizi, kumetokana na uzembe wa hali ya juu kwa mamlaka
zote zinazohusika na usalama wa majini kwa vyombo ya usafiri, hususani hawa jamaa
wa SUMATRA. Matukio ya kuzama kwa meli hizi mbili kunafanana kabisa. Ni vyema matamshi
na kauli zao zikawa zinatathmini matukio haya yanayoendana na usalama wa abiria.
SUMATRA walijitetea kuwa hawahusiki kwa upande Zanzibar, lakini watambue
kuwa wanahusika na usafiri wa majini. Kuhusika wanahusika tu kwa sababu
watanzania wengi walipoteza maisha yao, huku wao wakikwepa majukumu ya msingi. Kifupi,
SUMATRA hawana jipya kwenye sekta hii ya usafirishaji wa abiria. Wanachofanya
ni kujinufaisha tu. Kama wanapinga, hebu nenda pale Ubungo Bus Terminal uone
hali ilivyo. Kwa maisha ya sasa ya kisasa na kiteknolojia, tulitegemea Stendi
Iboreke kwa kuwa na Maeneo Mengi ya Kupunguzikia Abiria nyakati zote, za masika
na kiangazi, Viti vya kukaa abiria maeneo mbalimbali, angalau hata vile vilivyojengwa
kwa tofali na kusilibwa na simenti.
Majengo yaliyojengwa enzi ya Nyerere, yamebaki magofu, na sasa wameamua
kuegeshea magari. Stendi ni Chafu Mno. Ukiritimba, ubabe na unyanyaji na kupora
pesa za waendesha vyombo vya usafiri ndiyo dili. Wao wameegemea kusimamia pesa
tu za kwenye mabasi. Hawaangalie hali duni za stendi pamoja na huduma zake.
Cha Kusikitisha zaidi, leo tarehe 31 Agosti 2012, Mkurugunzi wa SUMATRA
bila hata aibu, ametangaza kuchukua hatua kwa mabasi ambayo yatachimba dawa
porini, bila kufikiri ni hatua gani wamezichukua toka Waziri wa Uchukuzi,
Mwekyemba alipotoa tamko. Huko porini, ardhi ni ya bure, mawe ni ya bora, miti
ni ya bore. SUMATRA wajiulizi ni shilingi ngapi wanazipora toka kwa Wamiliki wa
Mabasi ambazo zingejenga vyoo sehemu za mapori, ambapo abiria hujihudumia. Pia,
inabidi wajiulize, mtoto mdogo anaweza kusafiri masaa mawili bila kujihudumia?
Nadhani hawa wa jamaa wa SUMATRA wana familia, waongee kama binadamu wenye
utashi na si kubwatuka tu. Hii ni dhuluma kwa wananchi na wamiliki wa mabasi
walipa kodi.
Ninachoweza kujifunza hapa ni kushamiri kwa Rushwa ambayo kwa sasa imefikia
katika hatua ya kuwa 'RUSHWA YA MFUMO' kiingereza inaitwa SYSTEMIC CORRUPTION. Rushwa ya Mfumo inatengenezwa na kulindwa na
watu wenye mamlaka. Huuendeshwa kwa misingi ya kutoa matamko na maamuzi yasiyo na
fikra wala busara. Maamuzi mengi huwa ni kukurupuka tu bila kuangalia athari na
hatari ambazo zinaweza kujitokeza mbele. Rushwa ya Mfumo ni Hatari kwa sababu
husababisha kutoamika kwa watu wale ambao wanapaswa kutoa maamuzi mazito kwa
maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Maamuzi wengi yanayotolewa na Watendaji na Wanasiasa wasiojali maslahi ya
taifa na wananchi kwa ujumla yanakuwa katika misingi ya Rushwa ya Kimfumo. Ndiyo
maana pale mwanzo niliuliza, unaweza kumweka Mbuzi karibu/mdomoni mwa Simba na
ukategemea mbuzi huyo akaendelea kuwa hai? Haya ndiyo masuala ya msingi
tunapaswa kuhoji kabla ya kutoa matamko na matangazo kwa umma wa Watanzania.
Kitengo cha Naibu Waziri kuwaagiza Polisi na SUMATRA kufanya ukaguzi wa
vyombo vya usafiri kabla ya kupewa leseni za biashara ya kusafirisha biashara,
binafsi naona una walakini/tatizo kubwa. Idara Mbili hizo, binafsi zina imani
nazo. Pia, nimebaini kuwa zimeshindwa kuonesha weledi na umahiri katika
kusimamia huduma za usafirishaji wa abiria, pamoja na suala zima la haki za
abiri, usalama wake, na pia maslahi ya abiria wanapokuwa kwenye vituo vya
mabasi kabla ya kusafiri na baada ya kuwasili kwenye vituo vingine.
Kwa mfano, kushamiri na kukifiri kwa matuta kwenye barabara kubwa ambazo
zinasafirisha maelfu ya abiria ni hatari kubwa kwa usalama wa chombo chenyewe
na pia abiria waliomo ndani yake. Kisayansi, ukipima mtikisiko wa basi linaporuka
matuta makubwa na madogo kwa umbali wa kilometa 1000, madhara yake ni makubwa
mno. Lakini angalia hawa jamaa wanaojiita wasimamizi wa usalama na huduma ya
usafiri wa abiria wamekaa kimpya tu. Ni dhahiri, wanaangalia maslahi yao mengine na si usalama wa abiria.
Kwa kutumia kodi za Watanzania, hawa jamaa wanasafiri,
lakini hawajifunzi hata kidogo kwenye nchi za wenzetu. Usalama wa barabarani unaendana
na sayansi na teknolojia. Nenda tu hapo Afrika Kusini, unaona tofauti kubwa katika
nchi hizi za kiafrika. Kwa mfano, Alama za Barabara ni Kubwa mno na hazihitaji mtu
kuvaa miwani. Lakini Viashirio vya Barabara kupinda au tukio fulani muhimu huoneshwa
kwa Mabango Makubwa, huku umbali unaopungua kufikia tukio hilo, ukionekana kwenye
Alama hizo. Kama ulikuwa umbali wa mita 1000 utaendelea kupungua 800m, 600m, 400m,
200m, 100m, 50m. Tuna miti mingi, mbao ndio usisema, mawe ndio, basi, hata kama
hatuna chuma, hatuwezi kushindwa. Ka-Alama kabarabara ni kidogo, kimoja, kamejificha,
kamefutika. Yaani, ni hatari tu. je utegemee usalama hapa. Tujifunze.
Nimalizie kwa kusema kuwa Naibu Waziri unatoa
maelekezo na maamuzi katika mikono isiyo misafi, na utegemee kinyume na
matarajio yako, kama kweli ulikuwa na nia ya dhati ya kuwapa haki yao, abiria
maskini wa Kitanzania, ambao wamekuwa wahanga wa hii Rushwa ya Kimfumo.
Imendaliwa na:
No comments:
Post a Comment