Toleo la Kwanza - 2013
UKOO NI NINI?
Ukoo ni muungano wa
familia kadhaa zenye utambulisho fulani. Unaweza kuwa utambulisho wa jina,
alama au mwelekeo mmoja. Utambulisho wowote kati ya hizo nilizotaja, unaufanya
ukoo utambulike miongoni mwa jamii mbalimbali. Mara nyingi utambulisho ambao
huufanya ukoo utambulike baina ya jamii za Kiafrika ni Jina. Pamoja na jina, halikadhalika
kuna tunu (values) mbalimbali ambazo huheshimiwa na ukoo husika na jamii kwa
ujumla.
Tunu hubeba mambo mengi,
ikiwa ni pamoja na miiko, maadili, heshima, vyakula na tamaduni. Sambamba na
tunu, pia kuna Mila na Desturi, ambazo huzingatiwa sana katika masuala ya
kijamii, mfano wakati wa kuoa au kuoza, misiba, sherehe za jadi mfano matambiko
na masuala ya kimila.
Ukoo wa Kivenule ni
mmojawapo wa koo nyingi kubwa zilizopo katika Himaya ya Uhehe katika Mkoa wa
Iringa. Ukoo wa Kivenule ulianza kutambulika toka Karne ya 18. Historia
inaonesha kuwa Ukoo huu asili yake ni kutoka kwa Wabena-Manga, waliopo Kusini
mwa Mji wa Iringa; yaani maeneo ya Mufindi na Njombe. Ni mchanganyiko wa Wahehe
na Wabena wanaojulikana kama Wabena-Manga.
Wahehe ni moja kati ya
makabila makubwa hapa Tanzania ambalo kiasili linaishi katika Wilaya za Kaskazini
mwa Mkoa wa Iringa, yaani Iringa Vijijini, Iringa Mjini, Kilolo na Mufindi. Kwa
mujibu wa taarifa mbalimbali zinazopatikana na kutafitiwa, inasemekana kuwa ni
moja kati ya makabila yaliyotokea kwenye bonde la mto Rufiji; yaani Wahehe
wenye Asili ya Ungazija. Pengine hata ile sababu ya kuzika wafu wao wakielekea
mashariki inapewa uzito.
Lugha ya Kabila hili ni
Kihehe na limegawanyika kiasi fulani katika lahaja (matamshi) tofauti tofauti
kutokana na maeneo ambayo huzungumzwa. Inafanana kimatamshi na kimaana na lugha
ya Kibena iliyopo wilayani Njombe. Pamoja na Wabena wanaohesabika kuwa zaidi ya
watu milioni moja. Wengi wao ni wafuasi wa Ukristo, hasa wa Kanisa Katoliki
(Jimbo Katoliki la Iringa). Kihistoria Wahehe ni maarufu kwa jinsi
walivyopambana na Wajerumani walioteka maeneo yao, kama katika mapigano ya
Lugalo mwaka 1891. Kiongozi wao alikuwa Chifu Mkwawa.
Katika kuenzi na kutunza
tunu za asili za Uhehe, Ukoo wa Kivenule hauli nyama ya Mbawala (kwa lugha ya
Kihehe Mato/Imato). Imani kubwa imejengeka miongoni mwa jamii ya Ukoo wa
Kivenule kuwa kula Mbawala ni kuvunja miiko ya Ukoo ambayo iliyowekwa na
Waasisi wetu (Babu zetu). Mara mwanaukoo anapokiuka miiko hii na kula nyuma ya
Mbawala (Imato) basi huweza kufikwa na matatizo mbalimbali, mfano kudhurika
afya yake. Mara nyingi huwapata matatizo kama ya kuvimba miguu na pengine kuoza
kabisa.
Tunu nyingine ambazo Ukoo
wa Kivenule unazienzi kama zilivyo koo nyingine katika Uhehe ni Miitikio (Midikiso). Tunu hii huutambulisha Ukoo wa Kivenule
miongoni mwa Koo za Wahehe. Mwitikio (Mwidikiso) wa Ukoo wa Kivenule ni 'MLIGO'. Mwitikio huu hutumika katika maeneo
mbalimbali mfano katika salamu, kuapa (kufanya viapo) na pia kujitofautisha na
koo nyingine. Miitikio (Midikiso) huutambulisha Ukoo wa Kivenule katika koo
nyingine katika ardhi ya Uhehe.
CHIMBUKO LA UKOO WA KIVENULE
Kwa Asili, Ukoo wa Kivenule
ni maarufu kama Wapiganaji wa Vita. Ukoo wa Kivenule ulikuwa hodari sana katika
vita vya msituni ambavyo viliwahusisha Babu zetu akina TAGUMTWA. Enzi hizo za Mababu zetu vita za Koo na Kabila
zilipiganwa maeneo mengi ya himaya ya Uhehe kwa lengo la kupata mali, mifugo na
heshima.
Babu TAGUMTWA
BALAMA (KIVENULE) ndiye aliyewazaa Babu
TAVIMYENDA KIVENULE na Babu KALASI KIVENULE. Ikumbukwe kuwa,
jina halisi la ukoo wa Kivenule ni BALAMA.
Kama ilivyokwisha julikana katika mada iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa
Kwanza na wa Pili wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule, ambapo ilielezwa kuwa, neno KIVENULE linamaanisha sifa ya kuwa jasiri Vitani na hasa katika kutumia
silaha za Mishale na Mikuki yaani kwa Lugha Asilia ya Kihehe
“KUMIGOHA”. Yaani kwa maana nyingine LIGALU yenye maana ya Kwihoma
Imigoha – Kuhoma Watavangu au Kuvenula
Avatavangu. LIGALU maana yake Vita. Kuhoma maana yake Kuchoma na Migoha maana
yake Mikuki. Venula maana yake ua, fyeka
maadui.
LIGALU ndiyo iliyochangia kuzaliwa kwa jina la
Ukoo la KIVENULE. KIVENULE maana yake ni Ushujaa kutokana na Shabaha ya Mikuki.
KUVENULA likiwa na maana halisi ya kuwa na
shabaha ya kuwaangamiza maadui kwa kutumia silaha ya Mishale na Mikuki. Babu
zetu akina TAGUMTWA BALAMA
walilidhihirisha hili katika Vita na Watavangu na hivyo kusababisha kuzawadiwa
kwa jina la KIVENULE kama jina la sifa kutokana na ushujaa katika Vita.
Tagumtwa alijulikana kama anatoka Ukoo wa Balama na alikuwa
na Shabaha sana ya Mikuki katika uwanja wa Vita. Alikuwa hakosei shabaha (target) na hivyo hupelekea kuwaangamiza na kuwaua sana maadui.
Wakati akiwamaliza/fyeka/au adui zake kwa Mikuki, Wakuu wa Vita (Vatavangu)
walikiita kitendo hicho 'KUVENULA'.
Taarifa za Tagumtwa kuua (Kuvenula) adui zake katika uwanja wa vita, zilizagaa
kila mahali na hivyo kupelekea Wakuu (Viongozi) wa Vita (Vatavangu) kumzawadia
Jina la KIVENULE, kama jina la sifa na heshima kwa kuwa
shujaa wa Vita.
Ikumbukwa kuwa asili ya Ukoo
wa Kivenule ni kutoka katika ukoo wa BALAMA
(MWIBALAMA). Hawa ni ndugu wa karibu wa Kivenule kabisa na hawapaswi
kuoana. Koo za Mwibalama zinapatikana maeneo mengi katika Mkoa wa Iringa
hususani katika Wilaya za Mufindi,
Iringa Vijijini, Iringa Mjini na Kilolo; hali kadhalika kama ilivyo ukoo wa
kina Mwakivenule.
TAGUMTWA KIVENULE alifia katika uwanja wa mapambano (vita) na mwili
wake haukuweza kupatikana. Kama zilivyo koo za machifu au watu maarufu miili
yao ilikuwa haizikwi. Baada ya kufa iliegemezwa kwenye miti mikubwa na kuliwa
na wanyama. Wakija watu wasiukute mwili basi huamini kuwa mwili umechukuliwa na
Mungu.
KUKUA NA KUZAGAA KWA UKOO WA KIVENULE
Kwa mujibu wa taarifa
mbalimblai za kitafiti ambazo zimekuwa zikifanyika toka mwaka 2005 hadi sasa
2013; kupitia mikutano mbalimbali ya KAUKI; zinabainisha kuwa, BABU NYAKUDIRA BALAMA alimzaa BABU KANOLO BALAMA. Hali kadhalika
BABU KANOLO BALAMA alimzaa MTENGELINGOMA BALAMA.
Baada ya hapo, tunaona sasa
Kizazi cha TAGUMTWA KIVENULE
kinaanza kujitokeza. Hii ilikuwa ni Karne ya 18. TAGUMTWA KIVENULE alizaa
watoto wawili (2). Bado utafiti
unafanyika kumfahamu Mama wa watoto hawa. Watoto wa Tagumtwa Kivenule walikuwa
TAVIMYENDA KIVENULE na KALASI KIVENULE. Kwa mujibu wa taarifa kadhaa tulizonazo
kwa sasa; hawa ni vinara wa Ukoo wa Kivenule ulioenea maeneo mbalimbali hapa
Tanzania.
Tavimyenda Kivenule na
Kalasi Kivenule katika harakati za kutafuta maisha walifika katika eneo la
Kalenga, mahali alipoishi Mkwawa na kukutana na na Mwamyinga, aliyekuwa mfugaji
maarufu katika eneo la Ulefi huko Magubike, Iringa Vijijini. Tavimyenda
Kivenule alibahatika kupata kazi kwa Mwa-Myinga baada ya kuombwa kwenda
kumwangalizia mifugo yake huko Magubike, huku akimwacha mwenzake Kalasi pale
Kalenga.
Kalasi Kivenule yeye
hakupata fursa hiyo ya kazi na hivyo akaamua kuelekea eneo Irore katika Wilaya
Iringa Vijijini (kwa sasa Kilolo) kutafuta maisha. Huu ukawa ni mwanzo wa
kugawanyika kwa watoto hawa wawili wa Tagumtwa Kivenule.
Tavimyenda Kivenule
akielekea upande wa Magharibi mwa Mji wa Iringa na Kalasi alielekea upande wa
Mashariki mwa Mji wa Iringa.
Historia inabainisha kuwa
pamoja na Babu hawa kugawanyika kutokana na utafutaji wa maisha, mahusiano na
ushirikiano baina yao haukuvunjika. Babu zetu waliendelea kushirikiana na
kutembelea licha ya ukoo kukua na kuwa mkubwa sana.
KIZAZI CHA TAVIMYENDA KIVENULE
Katika Karne ya 19 hadi 20,
Kizazi cha Tavimyenda Kivenule kilizaliwa na kuzagaa katika maeneo ya Ulefi,
Magubike na Mlafu, Wilaya ya Iringa Vijijini, Iringa Mjini na maeneo mengine
mkoani Iringa.
Taarifa tulizonazo kupitia
tafiti tunazofanya, hali inaonesha kuwa, Babu Tavimyenda alikuwa na wake watatu
(3), ambao ni:
1. Bibi Mkami Sekabogo
2. Bibi Senosa
3. Bibi Pili
Mvemba
Mke wa kwanza wa Tavimyenda
Kivenule aliolewa akiwa na mtoto; aliyejulikana kama Bibi Sikimbilavi Semabiki.
Kwa mke huyu wa Kwanza Sekabogo, Tavimyenda alizaa nae watoto wanne (4); ambao
ni:
1. Babu Kavilimembe Kivenule
2. Babu Mgaifaida Kivenule
3. Babu Sigatambule Kivenule
4. Babu Hussein Kivenule (Bado yupo hai)
Kwa Mke wa Pili Bibi Senosa,
Babu Tavimyenda akizaa nae watoto watatu (3); ambao ni:
1. Babu Abdallah Kivenule
2. Bibi Sigungilimembe Kivenule
3. Bibi Malibora Kivenule
Watoto hawa wa Bibi Senosa
waliishi maeneo ya Kihesa katika Mji wa Iringa.
Kwa upande wa mke wa Tatu wa
Bibi Pili Mvemba; Babu Tavimyenda alizaa mtoto mmoja aliyejulikana kwa jina la
BIBI MGASI KIVENULE (aliishi
wapi). Babu Tavimyenda Kivenule amezikwa katika eneo la Ulefi.
Baada ya hapo kizazi hiki
kimeendelea kukua hadi hivi sasa Karne ya 21. **Angalia Chati kuonesha Muundo
wa Ukoo wa KIVENULE**
KIZAZI CHA KALASI KIVENULE
Kwa upande wa Kalasi
Tagumtwa Kivenule, kizazi hiki kilienea maeneo ya Nduli, Mgongo, Itagutwa,
Kigonzile, Igominyi na Irore. Taarifa zinaonesha kuwa, Babu Kalsi Kivenule
alikuwa na wake wawili (2); yaani:
1. Bibi Semsakwa
Mnonikilwa
2. Bibi Mnyamtage
Sekindole
Bibi Semsakwa Mnoni Kirwa
kwa Babu Kalasi Kivenule alizaa watoto wawili (2) ambao ni:
1. Bibi Cheilaje Nginasambula Kivenule
2. Gingilemesa Kivenule
Kwa bahati mbaya hakuna
taarifa zozote za hawa watoto wawili wa Kalasi.
Kwa upande wa Bibi Mnyamtage
Sekindole, Babu Kalasi Kivenule alizaa mtoto mmoja ambaye ni Salamalenga
Kahengula Kivenule. Bibi Mnyatage Sekindole awali alikuwa ameolewa kwa
Mwa-Mhumba na kuzaa nae mtoto mmoja aliyeitwa Bibi Mganga Semhumba na baadaye
kufariki. Baada ya hapo aliolewa na Kalasi ambapo pia alizaa mtoto mmoja tu
anayefahamika kwa jina la Salamalenga Kahengula Kivenule. * Angalia watoto wa
Kahengula katika Chati ya Muundo wa Ukoo wa Kivenule*
Kuna taarifa nyingi kutoka
kwa Babu Tavimyenda Kivenule na Kalasi Kivenule. Mwingiliano wa koo nao
unaonesha simulizi hizi. Kwa upande wa Tavimyenda mke wa Kwanza Bibi Mkami
Sekabogo alikuwa na mtoto wa kufikia, aliyejulikana kwa jina la Bi Sikimbilavi
Semabiki. Hatujapata taarifa rasmi kuhusiana na kizazi cha Bibi huyu, kama
ilivyotokea kuwa Sipanganakumtwa Mwilongo Regina Sematagi aliyekuwa mtoto wa
kufikia Bibi Semkonda mke wa Salamalenga Kahengula Kivenule.
Sipanganakumtwa Mwilongo
Regiona Sematagi amesaidia kueneza kizazi cha Ukoo wa Mnyavanu. Taarifa zaidi
na ukoo wa Mnyavanu upo katika Chati ya Chimbuko na Muundo wa Ukoo wa
Kivenule.**
TABIA YA KIZAZI CHA TAVIMYENDA NA KALASI KIVENULE
KUOA WAKE WENGI
Tabia nyingine ya kizazi
hiki cha Tavimyenda na Kalasi ilikuwa ni kuoa wake wengi. Kwa mfano Tavimyenda
pekee alikuwa na wake watatu. Hali kadhalika Kalasi naye alikuwa na wake
wawili.
Hali hii ya kuwa na mke
zaidi ya mmoja walirithi watoto wao. Kwa mfano watoto watatu wa kiume wa Tavimyenda
waliozaliwa kwa Bibi Mkami Sekabogo walioa wake wawili hadi watatu. Mtoto wa
kwanza wa Babu Tavimyenda Kivenule aliyejulikana kama Kavilimembe Kivenule
alikuwa na wake wawili (2). Mtoto wa tatu wa Bibi Mkamai Sekabogo,
aliyejulikana kwa jina la Sigatambule Matesa Kivenule, alikwa na wake watatu. Hali
kadhalika mtoto wa nne wa Bibi Mkami Sekabogo anayejulikana kama Hussein
Kivenule alikuwa na wake wawili. Mtoto pekee wa Pili wa Bibi Mkami hakubahatika
kuwa na familia; na alijiita jina la kujinyanyapaa "Mgaifaida"
Kivenule.
Sambamba na tabia ya Ukomo
wa Kivenule kuoa mke zaidi ya moja; pia kuna utamaduni uliojitokeza kwa baadhi
ya watoto wa Bibi Mkami Sekabogo kuoa dada na mdogo wake. Hili linajidhihirisha
kwa wake wawili wa Babu Kavilimembe Kivenule ambao walikuwa ni Bibi Sikumwendinguluvi
Sekusiga (Bi Mkubwa) na Bibi Gakumwalia Sekusiga (Bi Mdogo).
Hali kadhalika kwa mtoto wa
tatu wa Bibi Mkami Sekabogo; Babu Sigatambule Matesa Kivenule alioa wake
watatu, ambapo wake wawili wakubwa, 'Bibi Sikumwendinguluvi Singaile (Bi
Mkubwa) na Bibi Nyanyilemale Singaile (Bi Mdogo wa Pili); na wa tatu aliitwa
Bibi Pangulimale Setwanga.
Mtoto wa nne wa Bibi Mkami
Sekabogo Hussein Kivenule, yeye alioa wake wawili kutoka familia tofauti. Wake
zake waliitwa Bibi Yimilengeresa Semsisi (Bi Mkubwa) na Bibi Dalika Setala (Bi
Mdogo). Kwa upande wa watoto Kalasi Kivenule, mtoto wake Salamalenga Kahengula
Kivenule naye alioa wake watatu; ambao ni Bibi Semkonda, Bibi Semfilinge na
Bibi Nyangali.
Hatujapata taarifa rasmi za
watoto wa Kalasi kutoka kwa mke wake Bibi Semsakwa Mnonikilwa ambao ni Cheilaje
Nginasambula Kivenule na Gingilemesa Kivenule. Kwa upande wa Kahengula yeye
alioa kutoka katika familia tofauti.
UZAO WA BABU KAVILIMEMBE,
MGAIFAIDA, SIGATAMBULE NA HUSSEIN KIVENULE
Babu Kavilimembe Kivenule
aliishi eneo la Magubike, Wilaya ya Iringa Vijijini, huku akipakana na Ulefi
upande wa Kaskazini, Idete na Ibogo upande wa Magharibi. Akiwa ameoa wake
wawili wa familia moja, Babu Kavilimembe alibahatika kupata watoto sita (6).
Kwa upande wa mke wa kwanza
Bibi Sikumwendinguluvi Sekusiga; Mzee Kavilimembe Kivenule alipata watoto
wafuatao:
1. Elizabert Kivenule
2. Dalikimale Kivenule
3. Sandra Kivenule
4. Pangalasi Kivenule
Na kwa mke mdogo Bibi
Gagumwalia Sekusiga, Mzee Kavilimembe alipata watoto wawili ambao ni:
1. Salikuvaganga Kivenule
2. Francis Kivenule
Watoto hao wa Babu
Kavilimembe wengi wao waliishi maeneo ya Ulefu na Magubike. Baadhi yao walihamia
maeneo mengine kama Nzihi, ukiacha wale waliokuwa watumishi wa serikali
wakaenda kuishi maeneo mbalimbali. Babu Kavilimembe amezikwa eneo la Magubike,
Iringa Vijijini.
Kwa upande wa Babu Mgaifaida
Kivenule, yeye hakubahatika kupata familia. Mgaifaida alikuwa na ulemavu ambao
ulimfanya ashindwe kutembea katika hali ya kawaida. Muda mwingi aliishi eneo la
Ulefu kabla ya sehemu kubwa ya Ukoo wa Kivenule kuhamia sehemu ya Mlafu. Baada
ya kufariki, alizikwa Mlafu.
Babu Sigatambule Matesa
Kivenule alikuwa ni mtoto wa tatu wa Tavimyenda Kivenule kwa Bibi Mkami
Sekabogo. Babu Sigatambule aliishi Ulefi, akahamia Mlafu na baadaye Kidamali.
Babu Sigatambule ndiye aliyehakikisha Ukoo wa Kivenule unapata eneo la Mlafu
huku akipambana na Wagiriki. Walowezi na wawekezaji katika zao la Tumbaku.
Babu Sigatambule Kivenule
katika uhai wake alibahatika kuoa wake watatu (3); huku wake zake wawili
wakitoka katika familia moja ya ukoo wa Singaile. Wake zake hawa wakubwa
waliitwa Bibi Sivangumhavi Singaile na Bibi Nyanyilimale Singaile. Mke wa Tatu
wa Babu Sigatambule aliitwa Bibi Pangulimale Setwanga. Wote waliishi Mlafu na
baadaye kuhamia eneo Kidamali.
Wake zake wawili Bibi
Nyangilimale Singaile na Bibi Pangulimale Setwanga bado wapo hai na wanaishi
Kidamali.
Watoto wa Babu Sigatambule
Kivenule ni hawa wafuatao:
Kwa Bibi Sivangumhavi
Singaile (Mke Mkubwa):
1. Gidagumhindi Cecilia Kivenule
2. Semyamba Khadija Kivenule
3. Sivinitu Alphonce
Kivenule
4. Kadungu William
Kivenule
5. Fibumo Xavery
Kivenule
6. Mlagile Anyesi
Kivenule
7. John Kivenule
Bi. Gidagumhindi Cecilia Kivenule, mwaka 2012 alipotembelewa nyumbani kwake Magubike, Iringa Vijijini |
Bibi Nyanyilimale Singaile
(Mke wa Pili)
1. Mgulwa Agnes
Kivenule
2. Luhanage Ponsiano
Kivenule
3. Mgendwa Eusebio
Kivenule
4. Msinziwa Daniel
Kivenule
5. Kanolo Edward
Kivenule
Waliokaa kutoka kushoto ni Marehemu Luhanage Ponsiano Sigatambule Kivenule (Kidamali), Bernad Kivenule (Irore), Pius Kivenule (Irore) na Kivenule wengine kutoka Irore |
Mke wa Tatu wa Bibi
Pangulimale Setwanga
1. Conjeta Kivenule
2. Pyela Kivenule
3. Faustino Kivenule
4. George Kivenule
5. Carolina Kivenule
Babu Sigatambule Kivenule
alifariki mwishoni mwa miaka ya 90 na kuzikwa eneo la Mlafu, Kidamali - Iringa.
Mzee Hussein Tavimyenda
Kivenule alikuwa ni mtoto wa nne wa Bibi Mkami Sekabogo. Yeye aliishi eneo la
Ulefi na baadaye Mlafu. Kwa sasa anaishi Magubike. Babu Hussein Kivenule kwa
sasa anakadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 113 kwa mujibu wa taarifa na tafiti
ambazo tunazo.
Babu Hussein Tavimyenda
Kivenule ameshiriki kikamilifu katika Vita vya Pili ya Dunia. Wakati anashiriki
vita hiyo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 44. Amepigana vita maeneo mbalimbali
mfano Burma, India na Ulaya. Kwa sasa ana upofu wa macho ambao anasema ulisababishwa
na Baruti. Hali kadhalika anakiri kuwa kuendelea kuwa hai ni kwa sababu
alipigana upande wa Mwingereza. Anakiri vita ndiyo iliyomsababishia upofu
pengine asingekuwa na hali aliyonayo kwa sasa.
Mzee Hussein Kivenule alioa
wake wawili na kubahatika kupata watoto kumi na tatu (13). Kwa mke wake wa
kwanza Bibi Yimilengeresa Semsisi. Babu Hussein alipata watoto wafuatao:
1. Nyakudila Benjemin Kivenule
2. Sekiyavile Modesta Kivenule
3. Dominicus Kivenule
4. Emmanuel Kivenule
5. Luciana Kivenule
6. Ajendina Kivenule
Kwa upande wa mke wa pili wa
Bibi Dalika Setala, Mzee Hussein Kivenule alipata watoto wafuatao:
1. Kabogo Bernadi Kivenule
2. Sembata Josephine Kivenule
3. Necia Kivenule
4. Batromeo Kivenule
5. Brandino Kivenule
6. Tavina Kivenule
7. Masikitiko Kivenule
Asilimia kubwa ya familia ya
Babu Hussein Kivenule inaishi maeneo ya Magubike, Idete na Ibogo. Pia wapenda
historia mnakaribishwa kwenda kumtembelea Babu Hussein Kivenule.
UZAO WA SALAMALENGA KAHENGULA KIVENULE
Babu Salamalenga Kahengula
Kivenule alikuwa ni mtoto pekee wa kiume wa Babu Kalasi kwa mke wake wa pili
Bibi Mnyamtage Sekindole. Kahengula pia ni kaka wa Bibi Mganga Semhumba,
aliyekuwa mtoto pekee kwa Mwamhumba, aliyefariki mara tu baada ya kumzaa Bibi
Mganga kwa Sekindole.
Babu Salamalenga Kahengula
Kivenule alio wake watatu ambao ni:
1. Bibi Semkonda
2. Bibi Semfilinge
3. Bibi Nyangali
Salamalenga anapomuoa Bibi
Semkonda alimkuta na mtoto wa kufikia Sipanganakumtwa Mwilongo Regina Sematagi.
Kwa wake zake hawa watatu, Babu Salamalenga alibahatika kupata watoto kumi na
tatu (13). Kwa Bibi Semkonda alibahatika kupata watoto wafuatao:
1. Pangayena Kivenule
2. Jonas Kivenule
3. Samwel Kivenule
4. Galasamaneno Kivenule
5. Daud (William) Kivenule
6. Barton Kivenule
Kwa mke wa pili Bibi
Semfilinge, Babu Salamalenga alizaa nae watoto watatu ambao ni:
Chagovanue Kivenule
Munguatosa Kivenule
Mwilimilisa Kivenule
Na kwa mke wa tatu Bibi
Nyangali, Babu Salamalenga alizaa nae watoto wanne (4) ambao ni:
1. Tindasulanga Kivenule
2. Sigongola Kivenule
3. Shaban Kivenule
4. Gungamesa Kivenule
MWINGILIANO NA KOO NYINGINE KATIKA HIMAYA YA UHEHE
Zaidi ya Koo mbalimbali 50 zinachangamana
na Ukoo wa Kivenule. Hii ni kutoka Karne ya 18 ambapo kizazi hiki kilianza
kujitambua na kujikusanya. Baadhi ya Koo ambazo zimechangamana na ukoo huu ni
pamoja na koo za:
1. Kabogo
2. Kamtawa
3. Katowo
4. Kigereso
5. Kindole
6. Kisumbe
7. Kiteve
8. Kitu
9. Kusiga
10. Lawa
11. Luhwavi
12. Lupola
13. Madembwe
14. Manimu
15. Matagi
16. Mdongwe
17. Mfilinge
18. Mhapa
19. Mhumba
20. Mkeng'e
21. Mkonda
22. Mnonikirwa
23. Mnyavanu
24. Msisi
25. Mtono
26. Mvemba
27. Myalla
28. Ngeng'ena
29. Ngolo
30. Ngwenga
31. Ngweta
32. Nyakunga
33. Nyangali
34. Nyangalima
35. Mvemba
36. Nzala
37. Sambagi
38. Senosa
39. Setala
40. Singaile
41. Utenga