Siku ya Ijumaa, ya tarehe 10 Agosti 2012, nyakati
za asubuhi, ilikuwa ni siku ya ni masikitiko makubwa kwa Ukoo wa Kivenule,
watoto na familia yake kwa ujumla, baada ya kupata taarifa ya kifo cha Mzee
Ponsiano (Luhanage) Sigatambule, Tavimyenda Kivenule, kilichotokea katika Hospitali
ya Misheni ya Ipamba, inamilikiwa na Kanisa Katoliki. Hospitali hiyo ipo njiani
kuelekea Tosamaganga na Kalenga, Katika Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani
Iringa.
Historia yake ni ndefu, lakini kwa kifupi, Marehemu
Ponsiano Kivenule alizaliwa yapata miaka 69 iliyopita huko Mlafu, Kijijini
Kidamali. Katika uhai wake alifanya kazi kama Mwalimu na pia kama Bwana Mifugo.
Pia katika uhai wake amekuwa akiishi Kijijini Kidamali huku akishirikiana na
wenzake katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Baada ya kutokea kwa msiba huo, Uongozi wa Umoja wa
Ukoo wa Kivenule (KAUKI), kwa niaba ya Wana-KAUKI wote kutoka Kanda ya
Kidamali, Magubike, Nduli, Irore, Mufindi na Dar es Salaam, na wanaukoo kwa
ujumla, uliwatangazia taarifa hizo za Msiba Mkubwa wa Mzee Ponsiano Sigatambule
Tavimyenda Kivenule.
Pia taarifa hiyo, iliyotangazwa na Mwenyekiti wa
KAUKI, ilisema Mazishi ya Marehemu yatafanyika Kijijini Kidamali, Siku ya
Jumamosi ya tarehe 11 Agosti, 2012, katika Makaburi ya Mlafu, mnamo saa 7
mchana.
Marehemu Ponsiano Kivenule ameacha wake wanne na
watoto. Pia kama Wana-KAUKI, tumeachiwa pengo ambalo haliwezi kuzibika kutokana
na mchango wake mkubwa katika uanzilishi wa KAUKI na pia michango yake katika
Mikutano mbalimbali ya KAUKI ambayo amekuwa akihudhuria.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mahali Pema
Peponi, Amina.
Imeandaliwa na Kusambazwa
na:
Adam
Alphonce Kivenule