Wahehe ni moja ya kabila linalopatikana mkoani Iringa. Ni moja ya kabila ambalo limejiwekea historia kubwa hapa Tanzania. Inafafanuliwa kuwa kabila la Wahehe ni muunganiko wa makabila madogomadogo kama kabila la Wadongwe, na koo zingine kutoka Ng’uluhe na Lungemba, ambayo yalipata kukaa maeneo ya Iringa. Sababu ya muunganiko huo ni vita vilivyokuwa vikipigana kati ya Wahehe na Wasangu.
Kabla ya miaka ya 1860, hakukuwa na kabila lililofahamika
kwa jina la Wahehe, lakini mpaka kufikia
miaka ya 1860, kipindi ambacho wageni wanafika na kuandika habari za makabila
ya Tanzania, walipolipa jina kabila hili kuitwa Wahehe. Na asili ya jina hili
linatokana na namna ya makelele( Heee….heeee….heee…) waliokuwa wakiyapiga
wakati wa kwenda kwenye vita au hata wakati wa kupambana vitani.
Ufalme wa kihehe ambao uliopata kukua karne ya 19, ulitokana na uongozi wa chifu Munyigumba (Bunini au Mugohang’amwa) na mtoto wake Mkwawa. Inasimuliwa kuwa mnamo miaka ya 1850, ufalme wa wahehe au kabila hili la wahehe lilikuwa likiogopeka sana na makabila mengine kama Wasengo hata Wasangu pia.
Walikuwa wakiogopeka kutokana na kuwa na jeshi kubwa na
imara kama lile la mtemi Mirambo wa Urambo. Na mpaka wageni wanafika kwenye
miaka ya 1850/1860, Wahehe bado walionekana kuwa imara katika masuala ya
kivita. Kwani mpaka kufikia miaka ya 1870, Wahehe walifanikiwa kupigana na
kabila la Wamasai waliokuwa wametokea kaskazini-mashariki mwa Tanzania, ambao
nao pia walikimbia vita kutoka kwa
Wachaga na Wapare. Na zaidi ya hapo miaka hiyo hiyo ya 1870, wahehe walikuwa
wameshafanikiwa kutawala maeneo ya Dodoma hasa yale ya upande wa kusini na
kusini-magharibi. Hivyo sio tu makabila mengine waliowaogopa Wahehe bali hata
wageni hao waliwahofia sana Wahehe katika masuala ya kivita.
Kabila la wahehe wakiwa chini ya utawala wa Munyigumba,
walikuwa na mipango mingi ya kivita dhidi ya maadui zao. Na kwa wakati ule
Wasangu ndio walikuwa maadui wakubwa sana wa kabila la Wahehe. Na kwenye hiyo
miaka ya 1850, vita vilivyokuwa vikipiganwa vilikuwa kati ya Wahehe na Wasangu.
Wasangu ni moja ya kabila ambalo nalo lilionekana kukua kutokana na kuunganika
kwa koo mbalimbali zilizopata kuishi maeneo ya Iringa. Sababu kuu ya vita kati
ya Wahehe na Wasangu ni kwamba, kila kabila lilikuwa na sera yake ya upanuzi wa
eneo lao la utawala, na kila kabila lilihitaji kuteka makabila madogo madogo na
kuzifanya kuwa tawala zao. Hivyo kwenye hiyo miaka ya 1850 mapambano kati ya
Wahehe na Wasangu yalikuwa makubwa sana.
Lakini mambo yalikuja kubadilika mara baada ya Wangoni
kuingia katika ardhi ya Uhehe wakitokea maeneo ya kusini mwa Afrika(Rejea
historia ya Wangoni ilishaandikwa). Wangoni ambao walionekana nao kuwa imara
katika vita, kwani walisababisha maafa makubwa sana katika ardhi ya uhehe. Ujio
wa Wangoni kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Uhehe ulikuwa kwenye miaka ya
1870 na ujio wa mara ya pili ulikuwa miaka ya 1882. Hivyo mipango ya kivita ya
Wahehe, ikabadilika kutoka kwa Wasangu na kugeukia kwa Wangoni.
Na kuna uhakika kuwa, Wasangu waliamua kuungana na Wabena,
kwa lengo la kupambana na Wangoni walioonekana wakija kwa kasi kubwa sana. Na
wakati huo Wangoni wanafika katika ardhi ya Uhehe, walikuwa wameshagawanyika
kwenye makundi matano.
Kwa mara ya kwanza Wangoni na wahehe walipigana maeneo
ya Nyamurenge, ambapo Wahehe waliwapiga
Wangoni na kumuua kiongozi shupavu wa wangoni aliyefahamika kama Chipeta.
Kitendo cha Wahehe kumuua Chifu Chipeta ambaye ndie alikuwa kiongozi wa Wangoni
kwa upande ule, kilipelekea Wahehe kushinda vita.
Mbali na hapo mapambano mengine kati ya Wahehe na Wangoni
yalikuwepo maeneo ya Idete mnamo miaka ya 1870. Inafafanuliwa kuwa mapambano
kwenye hayo Wangoni walipigwa sana na hii ni kutokana na sababu ya njaa
walikuwa nayo. Kwani mtwa Mkwawa alitoa
amri kwa Wahehe wote kuhama na vyakula vyote na kuchoma moto mazao mengine.
Wahehe walifanya hivi kwa sababu walijua kuwa ujio wa Wangoni maeneo hayo
ulikuwa ni kutafuta chakula,, hivyo kitendo cha kuchoma moto mazao hayo ni moja
ya mbinu ya kuwashinda Wangoni.
Mapambano ya awamu hii kati ya Wahehe na Wangoni yalifika
mpaka maeneo ya Ndandu karibu na bwawa
la Itombololo. Mbali na Wangoni kufa kwa njaa, wengi wao walisukumwa kwenye
hilo bwawa na kufia mule. Na mwisho wa siku, mapambano kati ya Wahehe na
Wangoni yalipelekea kugawanyika kwa Ubena, yaani kukawa na Ubena ya kusini
chini ya Wangoni na Ubena ya kaskazini
chini ya Wahehe. Na mwisho wa siku yaani miaka ya1880 muunganiko kati ya
Wangoni na wahehe ukaanzia huko na utani kati ya Wahehe na Wangoni ukaanzia huko
Inafafanuliwa kuwa kwa kipindi chote hiko cha miaka ya
1870, Wahehe walikuwa chini ya uongozi wa Munyigumba.
Na mara baada ya kifo cha Munyigumba, mtoto wake ambaye
ndiye Mkwawa, alichukua madaraka na kuendeleza ufalme wa Wahehe. Inafafanuliwa
kuwa kifo cha Munyigumba kilisababishwa na mapambano kati ya Wahehe na Wabena
walioungana na Wandamba kutoka maeneo ya Kilombero. Vita kati ya Wabena na
Wahehe, Wabena na Wandamba waliongozwa na Mutengela kutoka kwenye ukoo wa
wakina Wakinamanga.
No comments:
Post a Comment