Sio washauri wazuri, wamejikita kwenye rushwa
tu
Nimekuwa nikitafakari mlolongo wa ajali ambazo
zimekuwa zikipurura maisha ya watu katika eneo la Mbalizi Mkoani Mbeya kwa wiki
sasa, tokea ajali mbaya iliyogharimu maisha ya watu zaidi ya kumi wiki
iliyopita. Ni masikitiko makubwa kwa sababu watu wale hawakupaswa kuondoka
mapema hivi. Hata ule usemi
wa mipango ya Mungu nashindwa kukubaliana nao kulingana mazingira ya ajali
hiyo.
Kwa wale mnaopenda kuperuzi habari mbalimbali zinazotokea hapa nchini,
mtakumbuka kuwa, siyo ajali ya mara ya kwanza kutokea katika eneo hilo, huku
ikihusisha mlolongo wa magari na wafu bila hata serikali kutoa suluhu la wimbi
la ajali ambazo zinaendelea kutokea katika eneo hilo.
Si ajabu ukasikia ari na amri ya kuwasihi wamiliki wa vyombo vya
usafirishaji kununua vipuri bora na vya kisasa na pengine kuwasisitiza kununua
magari yenye ubora! Lakini huku nyuma, wenye mamlaka ya udhibiti wa ubora wa
bidhaa mbalimbali mfano binadhaa na vyakula (Tanzania Bureau of Standard-TBS)
au wale wenzetu wanaosisitiza ubora wa huduma katika tasnia ya dawa na vyakula
(Tanzania Food and Drugs Authority-TFDA) ambao juzi juzi tu wamerasimisha dawa
feki za ARV zitumiwe na ndugu zetu wanaopunguza makali ya VVU, na kisha
kuendelea kusisitiza kuwa siyo dawa feki. Hii dhiyo taswira halisi ya Tanzania
tuliyonayo sasa.
Kama wenye mamlaka wanakiuka maadili ya taaluma zao na maadili ya kazi na
kuendelea kuangamiza Taifa, je kwa huyo mmiliki wa vyombo vya usafirishaji,
anayesutwa anunue vifaa/vipuri bora kwa ajili ya magari afanyeje? Ni dhahiri
kama nchi tupo katika janga kubwa la kuendelea kuathirika na majanga mbalimbali
ya kibinadamu.
Ukimwuliza mkazi wa Mbalizi kuhusiana na wimbi la ajali ambazo zinatokea
katika eneo hili, atakuambia kuwa jambo la kawaida kwa sababu ni kila wakati na
kila mwaka ajali mbaya na za kutisha zimendelea kushuhudiwa zikitokea mahali hapo.
Lakini tujiulize, kuna yeyote asiyejua changamoto za miundombinu katika
Mabonde ya Ufa. Kwa mfano eneo la Senkeke na Salanda katika Mkoa wa Singida;
safu ya milima ya Lukumbulo barabara ya kwenda Songea; Mlima Kitonga mkoani
Iringa, Wami Pwani na Nyang’olo Mtera, Iringa. Je, kuna yeyote ambaye hujui
kuwa katika kingo za bonde la ufa huwa na miinuko na miteremko mikali ambayo
huathiri miundo mbinu ya barabara na reli? Ni dhahili kwa wanataaluma na
wakandarasi wanayafahamu haya. Sijui kama wenzetu polisi, hususani wale wa
kitengo cha usalama barabara kama hufikiria tatizo la miundombinu katika maeneo
yaliyopitiwa na bonde la ufa.
Lakini pia kuna tatizo Kubwa la mlolongo na mlundikano wa matuta barabarani
(makubwa na madogo, yenye mtetemo mkubwa sana na wa kati, yenye ncha kali
na umbo lisiloeleweka) ambayo
yameendelea kuharibu magari pamoja na vipuri vyake. Ni kwa bahati mbaya gari
iliyohusika imeteketea kabisa. Pengine tungeweza kuona athari za matuta katika
vipuri vya gari hilo toka lilipoanza safari yake hapa jijini Dar es Salaam. Mathalani,
mifumo ya breki si imara kama wengi wetu tunavyodhani. Ipo macho ‘Sensitive’,
inaitika haraka ‘responsive’ na inawajibika ipasavyo ‘reactive’ pale inapoposwa
kufanya kama inaelekezwa. Kupita kwenye tuta za kina umbile kunachangia kwa
kiasi kikubwa kuvuga mifumo ya breki kwa kusababu kupasuka kwa mirija (pipes)
za upepo au vinginevyo ambayo inahusika na mifumo ya breki, pengine ndiyo ikawa
chanzo cha ajali nyingi zinazoendelea kutokea. Kwa kifupi, ajali za matatizo ya
mifumo ya breki kwa magari makubwa imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.
Mimi binafsi nilishuhudia kwa macho yangu busta za upepo wa breki kwa
matairi ya nyuma kwenye basi zikipasuka pale Mbuga ya Wanyama Mikumi, baada ya
basi kukanyaga matuta na hivyo kusababisha gari kukosa breki. Na safari
iliishia pale kwa sababu kulikuwa hamna namna nyingine. Kuna mifano mingi
ambayo imenikuta mwenyewe ikiwemo nyingine kuchomoka kwa boti upande wa kushoto
wa gari ndogo na hivyo kupelekea breki kupatikana kwa shida.
Pengine wenzetu hufikiria zaidi kukamata, kutisha na kupokea rushwa tu, na
si mambo ya kitaalam. Tukubaliane kuwa sera yao ni kushurutisha tu. Sioni
mantiki ya sababu zao za kila mara inapotokea ajali, ‘uzembe wa dereva’,
‘mwendo kasi’.
Mazingira ya ajali ya Mbalizi, kwa asilimia 90 linasababishwa na
miundombinu finyu (yaani inayobana) ambayo haiwezi hata kidogo kumpa fursa, dereva
wa gari ya aina yeyote ambaye atapatwa na tatizo la mifumo ya breki ya gari
kushindwa kufanya kazi. Ni dhahiri kabisa, kama breki zitashindwa kufanya kazi,
huna jinsi kulingana na barabara ilivyo na mazingira halisi ya kuweza kujiokoa.
Tofauti na miinuko mingine kama Kitonga ambapo mara nyingi maderera wameweza
kujiokoa kwa kuparamia gema ambazo zipo karibu mno na barabara.
Barabara ya mbalizi ni mteremko mkali, usio na kingo au kizuizi chochote
cha kumwezesha dereva kujiokoa zaidi ya kuendelea kuifuata barabara mpaka hapo
atakapoweza kusimama salama au kinyume chake. Nina mfano mdogo tu ambapo siku
ya Jumamosi ya tarehe 06 Oktoba 2012, basi la Bajeti likiwa linaelekea Dar es
Salaam, dereva wake aliweza kuliokoa lisitumbukia bondeni katika eneo la Kitonga
baada ya breki zake kushindwa kufanya kazi na kulielekeza kwenye gema ambazo
abiria wote walipona. Hapa ni Kitonga, lakini ingekuwa ni Mbalizi, tungesikia
maafa mengine tena.
Kwa nini nasema ajali nyingi zinachangiwa na
polisi wetu? Nina sababu za msingi. Wakati magari aina ya toyota land cruizer
mwaka juzi yaliporipotiwa kupata ajali mfululizo, wachunguzi wa masuala ya ajali
ya magari huko Marekani, waliweza kubaini tatizo la kimakenika katika mifumo ya
breki na peda za breki katika magari hayo. Na kwa maana hiyo walimjulisha
mmiliki wa kiwanda kinachotengeneza magari hayo kuhusiana na tatizo hilo,
aliahidi magari yote ya modeli hiyo yarudishwe na pia kulipa fidia kwa wale
wote ambao waliathirika.
Siamini kama Tanzania nasi tulikuwa katika
mkumbo wa magari hayo mabovu na pengine hatukuchukua hatua zozote muhimu
kukabiliana na tatizo hilo. Sikuona sababu ya mwendo kasi na uzembe imetajwa
katika ajali nyingi zilizotokea ambazo zilihusisha magari hayo ya Toyota Land
Cruizer.
Tofauti na wenzetu hao weupe kutoa sababu za
msingi na kisomi, kwetu sisi sababu za ajali ambazo zinafahamika ni mwendo kasi
na uzembe. Na cha ajabu zaidi, nilisikia Kamanda wa Polisi wa Mbeya akisema
wanamtafuta Dereva wa gari iliyohusika katika ajali hiyo ili wamhoji. Sijui
kama alifariki au vinginevyo lakini sioni mantiki. Wao kama polisi, wanaojiita
Wataalam, wanasemaje kuhusiana na ajali hiyo, kwa kuhusianisha na ajali nyingi
ambazo zimetokea katika maeneo hayo.
Nasema kama nchi tuna janga la taaluma na weledi
katika kushughulikia majanga yanayotokea katika nchi yetu. Sidhani kama akili
ndogo inaweza kutawala akili kubwa. Ajali ni akili kubwa na tunapaswa kutumia
akili kubwa zaidi kutatua akili kubwa iliyopo ya wimbi na ongezeko la ajali za
barabarani.
Kwa mtazamo wangu, ufinyu wa miundo mbinu
katika mlima huo ndiyo chanzo cha ajali zote ambazo zimetokea katika eneo hili.
Jambo la msingi ni kupanua miundombinu na pia kuwepo barabara za dharura kwa
magari ambayo yanakuwa yamepata tatizo kufeli kwa mifumo ya breki. Barabara
hizo za dharura inabidi ziwe wazi muda wote na zitumike kwa dharura tu. Udongo
ni wa bure. Raslimali tunazo, kinachopaswa kuchuliwa ni hatua tu. Pengine
mnasubiri mpaka kiongozi wa juu wa serikali apoteze uhai katika eneo hilo ndio
mchukue hatua za kuboresha miundombinu. Nadhani damu za watanzania dagaa
haziwaumi na ndiyo maana hamchukua hatua za makusudi kuondoa tatizo hilo.
Imeandaliwa na:
Adam Kivenule
No comments:
Post a Comment