Ndugu Mpendwa,
YAH: OMBI LA TAARIFA MBALIMBALI KUHUSU
HISTORIA YA KABILA LA WAHEHE NA WABENA
Rejea kichwa cha habari hapo juu.
Uongozi wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) kwa heshima na taadhima, unakuomba
usaidie kutupa taarifa mbalimbali za Historia ya Wahehe na Wabena ili tuweze
kuzitumia wakati wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI, utakaofanyika kwa siku
mbili, Kijijini Kidamali, Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa; tarehe 29
hadi 30 Juni, 2013. Wakati wa mkutano, pia tutajadili hatua tulizofikia ili kuchapisha
kitabu cha Historia ya Wahehe ambacho kipo katika mchakato wa ukusanyaji
taarifa, na mada yake itawasilishwa katika mkutano huo na Mwalimu Israel
Mposiwa. Huu ni mfululizo wa mikutano ya KAUKI ambayo imekuwa ikifanyika maeneo
ya Kidamali mara 3, Irole mara 1, Nduli mara 1, Magubike mara 1, Igowole-Mufindi mara 1 na Dar es Salaam mara 1.
Uongozi wa KAUKI unaitambua kazi yako muhimu ya upashanaji habari na
thamani yake kwa jamii, na pia nafasi yako katika jamii na ushiriki katika
harakati mbalimbali za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo kwa kuhabarisha
jamii ya Watanzania.
Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI yanafanyika katika kanda za
Irole, Nduli, Itagumtwa, Mgongo, Idete, Nyamihuu, Kalenga, Wasa, Nyamahana,
Ilala Simba, Nzihi, Dar es Salaam, Kidamali, Magubike, Mufindi na kwingineko
ambako wanaukoo wanatoka. Maandalizi yanajumuisha michango ya fedha, mazao na mifugo
kwa wale ambao hawana fedha, yote ikiwa ni kwa ajili ya kutoa huduma za
chakula, maji, uchapishaji wa matini na barua, kabla na siku ya mkutano; na
usafiri toka Iringa Mjini hadi Kidamali; na Kidamali hadi Magubike kwa wageni
na wenyeji.
Kutokana na uzito wa jukumu hili, uongozi wa KAUKI, pia umeamua kuandika
barua rasmi ya kukualika katika mkutano huo. Ratiba na ramani vimeambatanishwa
pamoja na barua hii kwa taarifa zaidi.
Mipango ya KAUKI inajikita katika kujiimarisha katika ngazi zote za
kiutendaji, kiuendeshaji na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, kisiasa,
kimaendeleo na kimapinduzi.
Toka mwaka 2005 Mikutano ya KAUKI ilipoanza kufanyika, kumekuwa na
mwamko wa hali ya juu kabisa na wanaukoo wengi kutoka maeneo ya Iringa Vijijini
na kwingineko wamekuwa wakihudhuria na kujifunza mambo muhimu ya kimaendeleo.
Kwa wastani washiriki 160 na 180 toka zaidi ya vijiji 20 Wilaya ya Iringa
Vijijini, wamekuwa wakihudhuria katika siku mbili za mkutano na kupata mafunzo
mbalimbali kutokana na mada ambazo zimekuwa zikifundishwa.
KAUKI ina malengo mengi, lakini baadhi ya
hayo ni pamoja na:
·
Kuchapisha kitabu cha Historia ya Wahehe toleo la Kwanza: Ndani
ya kitabu kutakuwa na sehemu zifuatazo: Historia ya Wahehe na Kuibuka kwa Tawala na Koo mbalimbali ndani ya
Uhehe (Wanitole, Wahabeshi, Wangazija); Harakati za Mapambano ya
Kikabila na Himaya mbalimbali (Vita za Luhota; Mkwawa na Wajerumani; Mkwawa na
Mnyigumba; Mkwawa na Wabena, Wasangu na Himaya Mbalimbali; Sehemu ya Pili: Historia ya Koo za Wahehe: Chimbuko na
Historia ya Ukoo wa Kivenule [Mtengelingoma
Balama na akina Tagumtwa Kivenule], Vita za Vatawangu na Ushujaa wa Tagumtwa
katika Vita; Sehemu ya Tatu: Umoja
wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI); Mipango na Harakati zake katika kuwakwamua Wanaukoo
katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi, kutoka zaidi ya Vijiji 25 vya
Wilaya ya Iringa Vijijini;
·
KAUKI kuwa na ofisi yake
Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda zake ili kurahisisha
mawasiliano na utekelezaji wa mipango yake;
·
Kuisajili KAUKI na kuwa na
mfuko wa kusaidia wanaukoo katika elimu, afya, uchumi na matatizo mengine. Pia
kuchukua jukumu la utunzaji na uendelezaji wa historia ya Wahehe pamoja na
sehemu mbalimbali za kumbukumbu za mashujaa katika Wilaya ya Iringa Vijijini. Tayari
mfuko umeanzishwa na wanaukoo wanaombwa kuuchangia;
·
KAUKI kuwa na sanduku la
posta na tovuti. Tovuti (blog) yetu ya muda inapatikana kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com
·
KAUKI kufungua Akaunti
katika Benki. Akaunti tayari imefunguliwa na inajulikana kwa jina la: KAUKI,
Benki ya NMB, Akaunti Namba 6052301709, Tawi la
Mkwawa, Iringa Mjini;
·
KAUKI kuwa na vitendea kazi
mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti. Hii inatokana na kuongezeka kwa
kazi za KAUKI zinazohusisha kuandika na kuprinti sana. Kusudio la kuchapicha kitabu cha
historia ya Wahehe, kinahitaji vitendea kazi kama
kompyuta, printa, meza na viti;
·
KAUKI kuanza kutoa elimu
mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake. Elimu hiyo inalenga
kuifanya jamii kujitambua, uelewa katika masuala ya kiafya, umuhimu wa elimu,
ujasiliamali na kujengeana uwezo kwa kupeana uzoefu katika shughuli za
uzalishaji mali
ili kupunguza umaskini. Uzoefu unatolewa na wajumbe toka sehemu wanakotoka
hususani katika nyanja za uchumi, biashara, kilimo, elimu na uzalishaji mali;
·
KAUKI kubuni na kutekeleza
miradi ambayo itawasadia wanajamii. Kwa mfano Irole wamebuni na mradi wa kilimo
cha Alizeti na wanakusudia kuuanzisha. Taarifa zaidi zitatolewa kwenye mkutano
wa sita wa KAUKI. Jamii nzima tunapenda ijitambue na kutafuta namna ya
kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya
kiuchumi mfano kilimo cha mazao ya biashara na chakula; na
·
KAUKI kuwa na kitengo cha
utaalam, taaluma na ujuzi (teknolojia) ambacho kitafanya shughuli za kuwajengea
uwezo wana-KAUKI kupitia elimu, ushawishi, utetezi wa kisera na sheria mbovu;
kupunguza umaskini, magonjwa, ujinga na pia kuiletea fedha KAUKI kupitia
maandiko ya miradi (project proposal and appraisal), pamoja na miradi
mbalimbali ya ujasiamali. Suala hili lipo katika mchakato.
Baadhi ya kueleza hayo machache, napenda kutanguliza shukrani zangu
dhati, na natumaini utalikubali ombi letu.
Wako katika kazi,
Adam Kivenule
Katibu Mkuu - KAUKI