Mchakato wa Kuandaa Kitabu cha Chimbuko, Muundo na Historia ya Ukoo wa Kivenule na Uhehe kwa Ujumla

Mchakato wa Kuandaa Kitabu cha Chimbuko, Muundo na Historia ya Ukoo wa Kivenule na Uhehe kwa Ujumla
Karibu uone yale ambayo KAUKI inafanya

Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI, 2014

Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI, 2014
Chimbuko na Muundo wa Ukoo wa Kivenule (2005 - 2009)

Mkutano Mkuu wa10 wa KAUKI

Mkutano Mkuu wa10 wa KAUKI
Tangazo la Mkutano Mkuu wa 10 wa KAUKI

Thursday, 28 March 2013

OMBI LA TAARIFA ZA KABILA LA WAHEHE



Ndugu Mpendwa,

YAH: OMBI LA TAARIFA MBALIMBALI KUHUSU HISTORIA YA KABILA LA WAHEHE NA WABENA

Rejea kichwa cha habari hapo juu.

Uongozi wa Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI) kwa heshima na taadhima, unakuomba usaidie kutupa taarifa mbalimbali za Historia ya Wahehe na Wabena ili tuweze kuzitumia wakati wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI, utakaofanyika kwa siku mbili, Kijijini Kidamali, Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa; tarehe 29 hadi 30 Juni, 2013. Wakati wa mkutano, pia tutajadili hatua tulizofikia ili kuchapisha kitabu cha Historia ya Wahehe ambacho kipo katika mchakato wa ukusanyaji taarifa, na mada yake itawasilishwa katika mkutano huo na Mwalimu Israel Mposiwa. Huu ni mfululizo wa mikutano ya KAUKI ambayo imekuwa ikifanyika maeneo ya Kidamali mara 3, Irole mara 1, Nduli mara 1, Magubike mara 1, Igowole-Mufindi mara 1 na Dar es Salaam mara 1.
 
Uongozi wa KAUKI unaitambua kazi yako muhimu ya upashanaji habari na thamani yake kwa jamii, na pia nafasi yako katika jamii na ushiriki katika harakati mbalimbali za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo kwa kuhabarisha jamii ya Watanzania.

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Tisa wa KAUKI yanafanyika katika kanda za Irole, Nduli, Itagumtwa, Mgongo, Idete, Nyamihuu, Kalenga, Wasa, Nyamahana, Ilala Simba, Nzihi, Dar es Salaam, Kidamali, Magubike, Mufindi na kwingineko ambako wanaukoo wanatoka. Maandalizi yanajumuisha michango ya fedha, mazao na mifugo kwa wale ambao hawana fedha, yote ikiwa ni kwa ajili ya kutoa huduma za chakula, maji, uchapishaji wa matini na barua, kabla na siku ya mkutano; na usafiri toka Iringa Mjini hadi Kidamali; na Kidamali hadi Magubike kwa wageni na wenyeji.

Kutokana na uzito wa jukumu hili, uongozi wa KAUKI, pia umeamua kuandika barua rasmi ya kukualika katika mkutano huo. Ratiba na ramani vimeambatanishwa pamoja na barua hii kwa taarifa zaidi.

Mipango ya KAUKI inajikita katika kujiimarisha katika ngazi zote za kiutendaji, kiuendeshaji na kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, kisiasa, kimaendeleo na kimapinduzi.

Toka mwaka 2005 Mikutano ya KAUKI ilipoanza kufanyika, kumekuwa na mwamko wa hali ya juu kabisa na wanaukoo wengi kutoka maeneo ya Iringa Vijijini na kwingineko wamekuwa wakihudhuria na kujifunza mambo muhimu ya kimaendeleo. Kwa wastani washiriki 160 na 180 toka zaidi ya vijiji 20 Wilaya ya Iringa Vijijini, wamekuwa wakihudhuria katika siku mbili za mkutano na kupata mafunzo mbalimbali kutokana na mada ambazo zimekuwa zikifundishwa.
  
   KAUKI ina malengo mengi, lakini baadhi ya hayo ni pamoja na:
·         Kuchapisha kitabu cha Historia ya Wahehe toleo la Kwanza: Ndani ya kitabu kutakuwa na sehemu zifuatazo: Historia ya Wahehe na Kuibuka kwa Tawala na Koo mbalimbali ndani ya Uhehe (Wanitole, Wahabeshi, Wangazija); Harakati za Mapambano ya Kikabila na Himaya mbalimbali (Vita za Luhota; Mkwawa na Wajerumani; Mkwawa na Mnyigumba; Mkwawa na Wabena, Wasangu na Himaya Mbalimbali; Sehemu ya Pili:  Historia ya Koo za Wahehe: Chimbuko na Historia ya Ukoo wa Kivenule [Mtengelingoma Balama na akina Tagumtwa Kivenule], Vita za Vatawangu na Ushujaa wa Tagumtwa katika Vita; Sehemu ya Tatu: Umoja wa Ukoo wa Kivenule (KAUKI); Mipango na Harakati zake katika kuwakwamua Wanaukoo katika lindi la umaskini, ujinga na maradhi, kutoka zaidi ya Vijiji 25 vya Wilaya ya Iringa Vijijini;
·         KAUKI kuwa na ofisi yake Kijijini Kidamali na pia sehemu nyingine za Kanda zake ili kurahisisha mawasiliano na utekelezaji wa mipango yake;
·         Kuisajili KAUKI na kuwa na mfuko wa kusaidia wanaukoo katika elimu, afya, uchumi na matatizo mengine. Pia kuchukua jukumu la utunzaji na uendelezaji wa historia ya Wahehe pamoja na sehemu mbalimbali za kumbukumbu za mashujaa katika Wilaya ya Iringa Vijijini. Tayari mfuko umeanzishwa na wanaukoo wanaombwa kuuchangia;
·         KAUKI kuwa na sanduku la posta na tovuti. Tovuti (blog) yetu ya muda inapatikana kupitia www.tagumwafoundation.wetpaint.com    
·         KAUKI kufungua Akaunti katika Benki. Akaunti tayari imefunguliwa na inajulikana kwa jina la: KAUKI, Benki ya NMB, Akaunti Namba 6052301709, Tawi la Mkwawa, Iringa Mjini;
·         KAUKI kuwa na vitendea kazi mfano Kompyuta, Printa, Simu, Meza na Viti. Hii inatokana na kuongezeka kwa kazi za KAUKI zinazohusisha kuandika na kuprinti sana. Kusudio la kuchapicha kitabu cha historia ya Wahehe, kinahitaji vitendea kazi kama kompyuta, printa, meza na viti;
·         KAUKI kuanza kutoa elimu mbalimbali kwa wadau wake. Inatoa elimu katika mikutano yake. Elimu hiyo inalenga kuifanya jamii kujitambua, uelewa katika masuala ya kiafya, umuhimu wa elimu, ujasiliamali na kujengeana uwezo kwa kupeana uzoefu katika shughuli za uzalishaji mali ili kupunguza umaskini. Uzoefu unatolewa na wajumbe toka sehemu wanakotoka hususani katika nyanja za uchumi, biashara, kilimo, elimu na uzalishaji mali;
·         KAUKI kubuni na kutekeleza miradi ambayo itawasadia wanajamii. Kwa mfano Irole wamebuni na mradi wa kilimo cha Alizeti na wanakusudia kuuanzisha. Taarifa zaidi zitatolewa kwenye mkutano wa sita wa KAUKI. Jamii nzima tunapenda ijitambue na kutafuta namna ya kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi mfano kilimo cha mazao ya biashara na chakula; na
·         KAUKI kuwa na kitengo cha utaalam, taaluma na ujuzi (teknolojia) ambacho kitafanya shughuli za kuwajengea uwezo wana-KAUKI kupitia elimu, ushawishi, utetezi wa kisera na sheria mbovu; kupunguza umaskini, magonjwa, ujinga na pia kuiletea fedha KAUKI kupitia maandiko ya miradi (project proposal and appraisal), pamoja na miradi mbalimbali ya ujasiamali. Suala hili lipo katika mchakato.

Baadhi ya kueleza hayo machache, napenda kutanguliza shukrani zangu dhati, na natumaini utalikubali ombi letu.
  
   Wako katika kazi,


   Adam Kivenule
   Katibu Mkuu - KAUKI

No comments:

Post a Comment