Wahehe mnamo 1906
Mkwawa au kwa jina refu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga
(1855 – 19 Julai 18981)
alikuwa chifu na
kiongozi mkuu wa kabila la Wahehe katika Tanzania ya leo wakati wa upanuzi wa ukoloni wa
Ujerumani mwishoni mwa karne ya 19.
Mkwawa ni maarufu hasa kwa kuongoza vita
vya Wahehe dhidi ya Wajerumani.
Upanuzi wa Wahehe
Jina la Mkwawa ni kifupisho cha Mukwava ambalo
tena ni kifupisho cha Mukwavinyika, lililokuwa jina lake la heshima
likimaanisha "kiongozi aliyetwaa nchi nyingi".
Mkwawa alizaliwa mnamo mwaka 1855 mahali palipoitwa Luhota karibu na Iringa mjini. Alikuwa mtoto wa chifu Munyigumba
aliyeaga dunia mwaka 1879.
Babake Munyingumba aliwahi kuunganisha temi ndogo za
Wahehe na makabila ya majirani kuwa dola moja. Aliiga mfumo wa
kijeshi wa Wasangu waliowahi kuwa kabila lenye nguvu kwa
kujifunza mfumo huu kutoka kwa Wangoni na impi za Shaka Zulu.
Hadi miaka ya 1870 eneo la
Wahehe lilipanuliwa mbali kuanzia kusini hadi katikati ya Tanzania ya leo.
Baada ya kifo cha chifu mzee watoto wake walishindania
urithi wake, na Mkwawa alishinda akawa kiongozi mpya.
Aliendelea kupanua utawala wake. Hadi mwisho wa miaka ya 1880 alitawala sehemu muhimu za njia ya
misafara kati ya pwani na Ziwa Tanganyika. Misafara hiyo ambayo ilikuwa
ikibeba bidhaa
za nje kama vitambaa, visu na silaha kutoka pwani, ikirudi na watumwa na pembe za
ndovu, ilipaswa kumlipia hongo
ikanunua pia wafungwa wa vita vyake. Hapo athiri na uwezo wake wa kulipa jeshi
kubwa ikaongezeka.
Mkwawa na upanuzi wa Wajerumani
Tangu mwaka 1885 hivi Wajerumani walianza
kuunda koloni lao katika afrika ya
Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika pamoja na Rwanda na Burundi) za leo).
Mwaka 1888/1889
utawala wao ulitikiswa na vita ya Abushiri lakini baada ya kushinda upinzani
wa Waafrika wa pwani Wajerumani walilenga kuimarisha
utawala wao juu ya sehemu za bara.
Mkwawa aliwahi kusikia mapema habari za Wajerumani
akajaribu kuwasiliana nao lakini bila kuelewana. Hapo aliamua kujenga boma imara
lenye kuta za mawe kwenye makao makuu yake huko Kalenga karibu na Iringa.
Katika mwezi Februari 1891
alituma wajumbe kwa kambi la Wajerumani huko Mpwawa
wakapokewa na gavana Mjerumani. Wakati huohuo Mkwawa aliendelea
kutuma askari
zake hadi Usagara iliyotazamwa na Wajerumani kama eneo lao.
[1]
Katika kipindi hicho gavana mpya Julius von Soden alifika
Dar es Salaam. Hakuwa na mamlaka juu ya mkuu mpya
wa jeshi Emil von Zelewski
aliyepokea amri zake kutoka Berlin moja kwa moja. Baada ya
kusikia habari za mashambulio ya Mkwawa katika Usangara aliomba na kupata
kibali cha "kuwaadhibu Wahehe".
Mapigano ya Lugalo
Katika mwezi Julai 1891 von Zelewski aliongoza kikosi
cha maafisa Wajerumani 13 na askari Waafrika hasa kutoka Sudan
320, pamoja na wapagazi 113. Walikuwa na bunduki za kisasa, bunduki za mtombo na mizinga midogo. Zelewski aliwadharau Wahehe kama
washenzi ambao walikuwa na mikuki na pinde tu. Kwa hiyo hakuona haja ya kutuma
wapelelezi wa awali.
Njiani aliangamiza vijiji alivyokuta na katika mwezi
Agosti alipoona Wahehe 3 waliomkaribia aliagiza kuwaua bila kuongea nao. Kumbe
walikuwa mabalozi
wa Mkwawa aliyetaka kujadiliana na Wajerumani.
Emil von Zelewski, kiongozi Mjerumani wa Lugalo
|
Tarehe 17 Agosti 1891 Zelewski
na jeshi lake walipita kwenye manyasi marefu karibu na Lugalo. Mkwawa alikuwa alimsubiri na Wahehe 3,000
walionyamaza hadi Wajerumani waliotembea kwa umbo la safu ndefu
walipokuwa karibu kabisa wakawashambulia.
Wajerumani walikosa muda wa kuandaa silaha zao
wakashtushwa kabisa. Sehemu kubwa ya askari waliuawa katika muda wa dakika chache pamoja na jemadari
von Zelewski. Sehemu ya kombania
ya nyuma ilirudi nyuma na kusimama kwenye kilima kidogo
walipoweza kutumia bunduki la mtombo wakajitetea na kuua Wahehe wengi. Sehemu
hii ilijumlisha maafisa 2 na maafande 2 Wajerumani waliweza kukimbia na
kujiokoa pamoja na askari 62 na wapagazi 74.
Kipindi cha vita
Baada ya mapigano Mkwawa alihesabu wafu wake waliokuwa
wengi. Alikataza mila za kilio kwa sababu alitaka
kuficha idadi ya askari waliokufa. Akielewa sasa kwamba silaha za Wazungu
zilikuwa hatari alituma tena mabalozi kwa gavana von Soden walioeleza ya kwamba
Wahehe walikuwa walijihami tu dhidi ya shambulio
na walitaka amani.
Lakini madai ya Wajerumani yalikuwa magumu, eti
kuwaruhusu wafanyabiashara kupita bila matata na kutoshambulia majirani tena.
Mkwawa hakuwa tayari kuahidi yote akachelewesha mikutano.
Wakati huo kamanda mpya Mjerumani Tom von
Prince alijenga boma jipya la Wajerumani katika Uhehe na
Mkwawa alijibu kwa kusambulia vikosi vidogo vya jeshi la kikoloni. Gavana Soden
alidai kutoendelea na mapigano. [2], lakini mwaka 1893
aliondoka Afrika, na gavana mpya von Schele alitaka kulipiza kisasi
akaamuru mashambulio dhidi ya Mkwawa.
Anguko la Kalenga
Mwezi Oktoba 1894
von Schele aliongoza kikosi cha maafisa Wajerumani 33 na askari Waafrika pamoja
na wagajai zaidi ya 1000 kuelekea Kalenga. Walikuwa na mizinga 4 na bunduki bombomu.
Walipofika mbele ya Kalenga Wahehe walijisikia salama
kutokana na kuta imara lakini Wajerumani walijipanga kilomita kadhaa nje ya mji wakaanza kufyatulia
mizinga yao na kuua watu ndani ya mji.
Wakati wa giza kwenye asubuhi wa tarehre 30 Oktoba 1894 askari wa jeshi la Schutztruppe walipanda ukuta
katika sehemu uliyodhoofishwa tayari na kuingia mjini. Hadi jioni walikuwa
wameteka mji wote.
Gombora na mikuki ya Wahehe hazikuweza kushindana na
bombomu za Wajerumani. Mkwawa mwenyewe aliamua kukimbia pamoja na askari 2000 -
3000, lakini kabla ya kukimbia alimwua mganga mzee
aliyewahi kutabiri ya kwamba atawashinda Wajerumani waliokuja.
Gavana von Schele aliandika taarifa kwa serikali ya Ujerumani "tulizika maadui 250, wengine walichomwa
katika nyumba zao, wanawake na watoto 1500 kutekwa nyara"
[3].
Mkwawa alijificha msituni
pamoja na askari zake akasubiri. Gavana von Schele alishindwa kuendelea na
mashambulio kwa sababu gharama
za vita zilishinda makisio yake na wabunge
wa upinzani katika Reichstag huko Berlin walipinga vita vya kikoloni; walikataa
kuongeza makisio na kiongozi wa wasoshalisti Agosti Bebel
aliita mtindo wa kuchoma mji na kuteka nyara watoto na wanawake "ushenzi
mkuu".
Amani fupi
Baada ya kuondoka kwa Wajerumani, Mkwawa aliweza kurudi
na kujenga tena nyumba mahali pa Kalenga.
Mnamo Septemba 1895
Mkwawa alikuwa tayari kujadiliana na Wajerumani na tarehe 12 Oktoba walipatana amani.
Wajerumani walimkubali Mkwawa kama chifu wa Wahehe, Wahehe waliahidi kukabidhi gobori zote, kupandisha bendera ya Ujerumani na kuwaruhusu
wafanyabiashara na wasafiri kupitia Uhehe. Mkwawa alimwagiza mjomba wake
kutia sahihi
akakataa mwenyewe akisema hii ingemwua.
Hata hivyo miezi kadhaa baadaye alitafuta msaada wa
Wajerumani kwa shambulio dhidi ya Wabena.
Afisa
mmoja Mjerumani aliyefika Kalenga mpya alizuiliwa kuingia na kumwona chifu akaambiwa
alipe hongo ya bunduki 5 ili kuingia katika eneo la Mkwawa. Hapo maafisa wa
jeshi la Wajerumani waliolinda mpaka,
ambao bado walikuwa wakitafuta nafasi ya kulipiza kisasi cha Lugalo, walidai
kuwa chifu amevunja mkataba.
Kapteni Tom von Prince alijenga boma jipya karibu na
Kalenga alianza kuwasiliana na machifu wadogo wa Wahehe. Mkwawa alijaribu
kujenga mapatano na majirani lakini Wabena na makabila mengine walikumbuka vita
na mashambulio ya awali kutoka Uhehe walipendelea kushikamana na Wajerumani.
Mkwawa aliwaua machifu wawili Wahehe waliowahi kukaa na
von Prince, lakini aliona hawakuwa peke yao kusita kumtii tena. Alipata habari
ya kwamba hata mdogo wake Mpangile alishikamana na Wajerumani.
Wakati wa Septemba 1896
Wahehe waligawanyika na sehemu kubwa ya viongozi waliochoka vita ilikuwa tayari
kuwakubali Wajerumani.[4]. Wajerumani waligawa eneo lao. Wasangu walirudishwa
katika eneo lao la awali wakarudi kutoka Usafwa
katika mji mkuu wa Utengule Usangu.
Mpangile alisimikwa kama kiongozi mpya wa Uhehe penyewe, lakini baaa ya siku 50
alisimamishwa na kuuwa na Wajerumani waliomshtaki, eti anamsaidia kaka yake
kisiri.
Katika maficho na kifo
Mkwawa alikuwa ameondoka sehemu za Iringa mwezi Agosti
1896 alipoona mgawanyiko. Alifuata mwendo wa mto Ruaha akilindwa na wenyeji waliokuwa tayari
kumficha na kumlinda dhidi ya vikosi vya Wajerumani waliomtafuta.
Mnamo Desemba 1896 alihamia milima
ya Uzungwa alipojificha. Kutoka huko alitelemka mara kwa mara kwenye
mabonde alipopata vyakula na kushambulia vikosi vidogo vya askari vya
Kijerumani.
Katika Julai 1897 kikosi kikubwa cha Wasangu
pamoja na Wahehe chini ya uongozi wa Wajerumani walikuta kambi la
Mkwawa mlimani wakalishambulia lakini Mkwawa aliweza kukimbia.
Mwaka 1898 Mkwawa aliendelea kujificha
kwenye misitu akiongozana na watu wachache sana. Aliishi hasa kwa njia ya
kuvinda.
Wakati wa Julai 1898 aliongozana na wavulana 4 pekee, halafu Wazungwa
2, mume na mke.
Tarehe 16 Julai Wajeumani waliowahi kusikia habari zake
walimkuta huyu mama Mzungwa alipotafuta chakula wakamkamata hata akawaambia Mkwawa alielekea
kusini. Wakamfuata na tarehe 18 Julai Mkwawa alimwua
mume Mzungwa kwa hofu ya kusalitiwa.
Aliendelea na wavulana 2 tu walioitwa Musigombo na
Lifumika. Watoto waliogopa angeweza kuwaua pia. Hapo Lifumika aliamua kukimbia
asubuhi ya tarehe 19 Julai. Lakini siku
ileile alipotelemka kutoka mlimani alikutana na kikosi cha Wajerumani akakimbia
lakini wakamshika wakamlazimisha kuwaambia habari za Mkwawa. Kijana alimwambia sajenti
Mjerumani kuwa chifu alikaa mgonjwa
mahali kwa umbali wa masaa 3. Walimlazimisha kuwaongoza. Njiani walisikia kwa
mbali sauti ya bunduki, risasi 1. Wakaendelea na baada ya masaa mawili walikuta
maiti za Mkwawa na yule kijana mwingine. Inaonekana waliwahi kujiua na
sauti ya bunduki ilikuwa Mkwawa aliyejipigia risasi.[5].
Fuvu la Mkwawa
Fuvu la Mkwawa katika Makumbusho
ya Kalenga karibu na Iringa, Tanzania.
Kichwa cha mtemi kinasemekana
kilikatwa na Wajerumani na kutumwa Berlin kilipohifadhiwa katika makumbusho, awali Berlin na baadaye Bremen.
Waingereza waliochukua
utawala wa koloni mwaka 1918 baada ya Vita Kuu ya Kwanza
ya Dunia walitaka kuonekana kama mabwana wema. Mkuu wa serikali ya
kikoloni ya Tanganyika alipendekeza
kurudisha fuvu kwa sababu Wahehe walishirikiana na Waingereza wakati wa vita.
Hivyo kuna kipengele 246 katika mkataba wa Versailles
kinachosema: "Katika muda wa miezi 6 baada ya kuthibitishwa kwa mkataba
huu ... Ujerumani utakabidhi fuvu la Sultani Mkwawa iliyohamishwa kutoka Afrika ya
Mashariki ya Kijerumani na kupelekwa Ujerumani kwa serikali ya Mfalme wa Uingereza."
Fuvu la Mkwawa katika Makumbusho ya Kalenga karibu na Iringa, Tanzania.
|
Lakini baada ya Vita vikuu vya pili
ambako Ujerumani penyewe ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza gavana Twining wa
Tanganyika alikumbuka habari za fuvu akatembelea Ujerumani na kutazama mafuvu
ya makumbusho ya Bremen.
Katika mkusanyiko wa mafuvu 2000, 84 yalikuwa na namba
zilizoonyesha yalitokea Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo aliyapanga
kufuatana na ukubwa na kutazama yale yaliyokuwa na vipimo vya karibu na ndugu
wa Mkwawa aliowahi kuwapima kabla ya safari yake. Hapo aliteua fuvu lenye shimo kwa
sababu taarifa ya kale ilisema Mkwawa alijiua kwa kujipiga risasi kichwani.
Fuvu hilo lilipelekwa Tanganyika tarehe 9 Julai 1954
na kuhifadhiwa katika jengo la makumbusho ya Mkwawa kwenye kijiji cha Kalenga.
Athari yake upande wa dini
Mkwawa alifuata dini za jadi, na alikataa ombi la Walutheri la kuanzisha misheni
Uhehe, lakini baadaye alikubali wamisionari Wabenedikto wa Kanisa Katoliki wahamie Tosamaganga
na kuanza kazi yao kati ya Wahehe.
Hata wakati wa vita vyake dhidi ya Wajerumani, Mkwawa
aliwaheshimu wageni wake hawa.
No comments:
Post a Comment