KATIBU wa Bunge, Thomas Kashilillah amepingana hadharani na bosi wake Spika
wa Bunge, Anne Makinda kuhusu kurushwa moja kwa moja matangazo ya Vipindi vya
Bunge.
Jana katika mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge,
Kashilillah alisema kuwa ofisi yake inakusudia kutoonyesha matangazo ya moja
kwa moja ya vikao vya Bunge vinavyofanyika mjini Dodoma kutokana na baadhi ya
wabunge kukiuka kanuni za kibunge kwa kuvunja maadili.
Hata hivyo, kauli ya Kashilillah inapingana na ile ya Makinda aliyoitoa
mjini Dodoma, Februari 8 wakati wa kuahirisha kikao cha 10 cha Bunge aliposema:
“Naipongeza TBC (Shirika la Utangazaji la Taifa) kwa kuonyesha moja kwa moja
matangazo na yote yanayoendelea bungeni.
“Kutokana na vurugu zilizotokea, ninaiomba Serikali kuiongezea ruzuku TBC
ili kupata mitambo ya kisasa waweze kuonyesha vizuri matangazo yake, safari hii
matangazo yalikuwa yanakatika katika sana,” alisema Makinda.
Hata hivyo, kauli hiyo wakati wa kufunga Bunge ilikuwa ni ya pili kwa
Makinda kwani baada ya kutokea vurugu zilizoongozwa na baadhi ya viongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Makinda aliisifu TBC kwa kuonyesha kila kilichotokea
bungeni na kuweka msisitizo kuwa lazima TBC isaidiwe ili kila kinachotokea
ndani ya Bunge kionekane kwa wananchi.
Akizungumza jana kwenye Ofisi za Bunge, Kashilillah alisema kuwa vikao
vinavyofanyika sasa mara nyingi vinakiuka kanuni na maadili ya shughuli za
Bunge, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wabunge kuinuka na kutoa kauli
mbalimbali wakati mijadala ikiendelea.
Kashilillah alisema, utaratibu unafanyika na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA), ili kuangalia namna ambavyo wataweza kuonyesha shughuli za Bunge kwa
vipande vipande vilivyorekodiwa kwa maeneo yanayofuata kanuni na maadili ili
kuficha taswira mbaya itakayojitokeza kwa wananchi.
“Kuna ukiukwaji mkubwa wa kanuni na maadili ya vikao vya Bunge, na si kwamba
wanaofanya hivyo hawafahamu, isipokuwa wanafanya makusudi au wanatafuta
umaarufu kupitia vikao hivyo. Kutokana na hali hiyo, tumeamua kukaa na TCRA ili
kuangalia namna ambavyo tunaweza kurusha vikao vilivyorekodiwa badala ya moja
kwa moja,” alisema.
Simu za matusi na kashfa
Akizungumzia suala la Spika Makinda kutukanwa na kukashifiwa, Dk Kashililah alisema kuwa, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ameshawafahamu wote waliofanya hivyo na taratibu za kuwakamata zinaandaliwa.
Akizungumzia suala la Spika Makinda kutukanwa na kukashifiwa, Dk Kashililah alisema kuwa, kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ameshawafahamu wote waliofanya hivyo na taratibu za kuwakamata zinaandaliwa.
“Tumeshawabaini, tunafahamu wanakoishi na namba zao tayari zimeanza
kushughulikiwa. Hasa wale wote waliotuma ujumbe wa matusi au kupiga simu,”
alisema.
Kuvunjwa kwa kamati
Kuhusu kuvunjwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge, alisema kuwa Spika wa Bunge anaweza kuzivunja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utendaji wake au ushauri unaotoka kwa viongozi wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Kuhusu kuvunjwa kwa baadhi ya Kamati za Bunge, alisema kuwa Spika wa Bunge anaweza kuzivunja kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utendaji wake au ushauri unaotoka kwa viongozi wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliangalia kamati ambazo zinafanya kazi kwa
mwingiliano na kuhamishia shughuli zile kwenye kamati nyingine kama ilivyokuwa
Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo shughuli zake zimehamishiwa
kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
No comments:
Post a Comment