WIKI
YA NENDA KWA USALAMA HAINA TIJA KATIKA KUPUNGUZA AJALI NA KUONGEZA WELEDI NA
UMAHIRI KATIKA KUTUMIA NA KUHUDUMIA WATUMIAJI WA VYOMBO VYA USAFIRI
Imekuwa ni kasumba kwa Jeshi la Polisi
hususani kitengo cha Usalama Barabarani kuonekana wakiwa barabarani
wakiwadhibiti madereva kuhusu zoezi la ukaguzi wa magari na leseni za udereva. Na
kwa bahati mbaya ukaguzi wa magari umekuwa ukiegemea zaidi kwenye magari ya
abiria na kuacha magari mengine watu binafsi yakiendelea kutembea mitaani.
Ukaguzi wa vyombo vya usafiri kama
magari ni muhimu kwa sababu kuna wamiliki wengine hujisahau na hivyo kushindwa
kuchukua hatua za makusudi kuangalia na kuhudumia magari yao. Lakini pia katika
ajali za barabarani magari yote huusika, yawe na binafsi au ya usafiri na kwa
maana hiyo, sheria lazima izingatiwe sawe kwa vyombo vyote vya usafiri.
Lakini kwa nini serikali haiweki nguvu
yake katika kushughulikia kwa mapana yake Wiki ya Nenda kwa Usalama Tanzania? Ni
dhahiri, viongozi hawana mwito au nia ya dhati katika kuhakikisha kuwa roho za
watanzania zinalindwa kutokana na wimbi kubwa la ajali za barabarani. Mara
nyingi najiuliza ni kwa nini hakuna bajeti maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa
watumiaji wote wa barabara na waendesha vyombo vya usafiri na watumiaji wake. Sijawahi
kusikia kutengwa kwa bajeti au fungu fulani kwa ajili ya kutoa elimu ya
msingi/mahususi kwa watumiaji wa magari, abiria na pia watumia barabara zetu.
Makampuni baki kwa maslahi yao, ndiyo
yameonekana kujitokeza kutoa fedha kiasi na nguo au baadhi ya vifaa kiduchu
ambavyo vinatumika wakati wa wiki hiyo moja tu ya nenda kwa usalama. Hii ni
kijeli na dharau kwa Watanzania ambao wengi wao wanaendelea kuumia kutokana na
lindi kubwa la ajili za barabarani zinazoendelea kutokea kila siku.
Binafsi naamini kabisa, kama serikali
kupitia jeshi la polisi, kitengo cha usalama barabarani wangeelekeza nguvu zake
katika kutoa elimu badala ya kujipanga barabarani kula rushwa, ajili nyingi
zinazoendelea kutokea, zingekoma kabisa. Madereva na
watumia barabara wangepata umahiri katika bahari hii ya usalama barabarani. Elimu
pekee ndiyo njia mahsusi ya kujikwamua na taifa hili na vifo na majanga ya
ajali.
Pia, kuendelea
kushamiri kwa matatu katika barabara zote za Tanzania ni chanzo kikuu cha
ajali. Na hii ni ishara ya kushindwa kwa jeshi la polisi na mamlaka nyingine
husika katika kusimamia matumizi bora ya barabara na watumiaji wake. Matuta
barabarani yanaendelea kudidimiza uchumi wa Tanzania kutokana na wananchi
kulipa fedha nyingi za kigeni kuagiza spea/vipuri vya magari yao. Mtikisiko
mkubwa ambao unalipata gari dogo, gari kubwa la mizigo na basi la abiria katika
umbali wa kilometa 1000, ni ishara kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja, gari
litakuwa limepunguza zaidi ya miaka miwili ya muda wake wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Matuta barabarani si suluhi ya
matatizo ya ajali yanayoendelea kutokea katika nchi ya Tanzania. Serikali,
polisi na mamlaka nyingine husika, zimeshindwa kabisa kutafuta suluhi ya
kuboresha usalama barabara na kuishia kuweka matuta. Hapa ndipo akili za wadau
wa usafiri zilipoishia. Hii ni aibu kwa taifa hili, hususani kwa wageni
mbalimbali wanaondelea kumiminika Tanzania.
Ukitembelea nchi za wenzetu kuna mambo
mengi ya kujifunza, mfano alama za barabarani huweka kwa kutumia mabanga
makubwa ambayo hayahitaji mtu kuvaa miyani kuyaona. Na pia huwekwa kila baada
ya umbali wa kilometa 1 au 2 huku humu katikati kukiwa na punguza la umbali wa
mita mia 200 hadi mia 300 kabla ya tukio halisi ambalo lilikuwa limelengwa. Mfano
kupinda kushoto kwenda mji mwingine, ambapo aina ya barabara na idadi ya
barabara huashiriwa katika mapango hayo elekezi ya usalafiri.
Tofauti na hapa kwetu, kibao cha
kuonesha kuwa unapaswa kutembelea kilometa 50 kwa saa huonekana ghafla tena kwa
maandishi madogo sana. Na pengine, unamkuta askari wa tochi amekaa hapo hapo na
kusema, umeovaspidi. Hii ni fedheha na ni aibu kwa taifa letu.
Naamini viongozi na watendaji
mbalimbali ambao ni wadau wa usafiri na usalama barabarani wanatembea mara kwa mara
katika nchi za wenzetu kwa nini hawaji na somo jipya.
Kauli mbinu na fulani hazina tija kwa
taifa letu katika tasnia ya usalama barabarani kama kutakuwa hakuna sera na
msingi mahsusi katika utoaji elimu na pia kuwaelimisha watumiaji wa barabara,
vyombo vya usafiri na vyombo vyenyewe.
No comments:
Post a Comment