Asili ya jina la
Iringa ni neno la Kihehe
"lilinga" lenye maana ya boma. Mji umejengwa juu ya mlima ukitazama
mto Ruaha
bondeni.
Mji uko kando la
barabara kuu ya Tanzania Zambia na kuna usafiri wa kila siku kwenda Dar es
Salaam na Mbeya.
Njia kwenda Dodoma
ni sehemu ya barabara ya kale ya "Cape-Cairo" kati ya Rasi ya Afrika
Kusini na Kairo
wa Misri lakini
kwa sasa ni barabara ya udongo tu.
Iringa
ilianzishwa mwaka 1892 kama kambi la jeshi la kikoloni wakati wa vita ya
Wajerumani dhidi ya Wahehe. Mji wa leo upo mahali pa "Neu Iringa"
au Iringa mpya ya Wajerumani waliotumia jina hili baada ya kuharibu boma la
mtemi Mkwawa huko Kalenga
waliloita "Iringa" tar. 31 Oktoba 1894.
KABILA la Wahehe ambalo linapatikana mkoani Iringa,
ni miongoni mwa makabila maarufu nchini ambalo halipo nyuma katika suala zima
la kuenzi Mila na Tamaduni zake.
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa
Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la
Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa,
Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao walioishi Udzungwa,
Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea
Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu
(Kihanga ya sasa), Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya
milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mbali na Kabila la Wahehe, Mkoa wa Iringa pia
unakaliwa na Kabila la Wabena, Wapangwa, Wawanji na Wakinga. Japo sasa una
mchanganyiko wa makabila mengine.
Kihehe ni lugha ya Kibantu nchini Tanzania
inayozungumzwa na Wahehe. Hali kadhalika,
Lugha ya Kihehe ya Kabila la Wahehe imegawanyika kutokana na Lahaja. Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo
hubainika kijamii au kijiografia. Lahaja za lugha moja zatofautiana katika
matamshi, miundo ya sarufi na msamiati. Kama lugha hutofautiana katika matamshi
tu, tofauti hizo huitwa lafudhi na siyo lahaja. Uchambuzi na uchanganuzi wa
lahaja ni tawi la isimujamii.
Pamoja na kuwepo kwa tofauti ya Lahaja, Wahehe wenyewe wanaweza kusikilizana bila tatizo
lolote ila huweza kutambua ni mahali gani Mhehe huyu anatoka mfano Wahehe
Vasungwa ambao wengi wao wanatoka eneo la Dabaga.
Suala la kuthamini tamaduni wanazorithi toka kizazi
kimoja hadi kingine, ni moja ya sababu zilizowafanya Wahehe wajizolee sifa
sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa sifa ambazo kabila hili limejizolea ni
pamoja na uvumilivu,
ujasiri,
uchapaji
kazi
ambapo kwao kilimo cha mazao ya chakula ni msingi mkubwa wa maendeleo katika
familia.
Anapobainika mtu mvivu, hudharauriwa na kuchekwa na ukoo
mzima pamoja na jamii inayomzunguka.
Baadhi ya mazao yanayolimwa mkoani humo ni pamoja na
mahindi, mtama, mihogo, alizeti, kunde, maharage, viazi vitamu, viazi mviringo,
karangaa na ulezi.
Katika kilimo, kabila hili hufanya ushirikiano kwa
namna ya kualikana baina ya mtu mmoja na mwingine na ushirikiano wa namna hii,
hujitokeza wakati wa kupalilia na kuvuna.
Ukifika wakati wa mavuno, mtu anayesaidiwa kazi kwa
siku hiyo huandaa pombe, togwa na kande kwa ajili ya wasaidizi wake. Kitendo
hicho cha kualikana katika kazi huitwa ‘Mugove’.
Kulingana na mila za kabila hilo, hususan katika
suala la kuandaa chakula, ni kwamba endapo mzazi mmoja atakuwa hayupo, mzazi
anayekuwepo humsubiri mwenzake ili aungane naye katika mlo. Hii mara nyingi
hufanyika kama kuna uhakika wa mzazi huyo kurudi mapema.
Hali ni tofauti
kwa watoto kwani endapo mtoto wa kiume au wa kike atakuwa hayupo bila sababu
maalumu, kimila haikubaliki hata kidogo kuwekewa chakula.
Chakula hicho ambacho huandaliwa na mwanamke au
msichana hugawanywa katika makundi matatu. Mafungu haya ni pamoja na fungu
la wazazi, wavulana na kundi la tatu ni
watoto wa kike.
Katika kabila hilo, afikapo mgeni hushikana mkono wa kulia na mwenyeji
wake na kila mmoja huanza kuubusu mkono wa mwezake kwa kupokezana mmoja baada
ya mwingine zaidi ya mara tatu na kitendo hicho huitwa ‘Kinonela’/Kwinonela.
Mhehe katika kufanya shughuli mbalimbali za
kimaendeleo, mara nyingi hupenda kujisimamia mwenyewe ambapo huamini kuwa
kusimamiwa ni kudhalilishwa au
kudharauliwa.
Kabila hili pia, bado lina imani za kishirikina
ambapo baadhi ya maeneo mkoani humo watoto wa vikongwe pamoja na ukoo wao
huogopwa kwa namna moja au nyingine, hususan katika suala la kugombea mashamba likiwemo la
wanafunzi.
Vile vile wanafunzi hushindwa kufanya vizuri katika
mitihani yao kwa kuhofia kufa. Siyo
hivyo tu, hata kufanya shughuli za maendeleo mfano kujenga nyumba nzuri
lilikuwa ni hatari sana siku nyuma, japo kwa sasa linapungua. Pengine mchanyiko
wa makabila umepunguza imani hizi na kuchochea maendeleo.
Pamoja na kuwaogopa vikongwe miongoni mwa kabila
hili huamini kuwa “Kufa konoga” wakimaanisha “kufa
kupendeza” .
Usemi huu wa 'kufa
kunoga' kwa Mhehe ni sehemu ya kujitia moyo na humuondolea hofu katika
kukabiliana na matatizo mbalimbali ambapo kufa kwao ni jambo la kawaida kama
ilivyopangwa na Mungu‘Nguluvi’.
Ugomvi mkubwa unaweza kutokea endapo mtu mmoja kutoka ukoo fulani atamnyooshea kidole mtu wa
ukoo mwingine kwa lengo la kumkemea ‘Kufingulisa’/kufingula.
Kitendo hicho kikitokea yule aliyenyoshewa kidole
huamini kuwa endapo atatokewa na baya lolote, litakuwa limetokana na yule
aliyemnyooshea kidole.
Kabila hili la Wahehe, pia lipo mstari wa
mbele katika suala la imani ambapo huomba baraka toka kwa Mwenyezi Mungu ili
kuweza kutatuliwa matatizo mbalimbali na kuomba neema na msamaha.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa Mzee
Albeto Lyakumba (63), kutoka
Kijiji cha Lungemba mkoani humo, katika kabila hilo mtu anapokufa ndugu zake
hawatakiwi kulia mapema mno, badala yake wanatakiwa kutulia kimya takribani saa
moja baada ya kifo hicho./ Hufanya hivyo kwa lengo la kupata muda wa kutosha
kuuweka vizuri mwili wa marehemu (maiti).
“Kitendo cha mtu kufa akiwa amekodoa macho au viungo
vyake havijakaa sawia huwa tunakilaani sana, hivyo tunatumia muda huo kuuweka
vizuri kwa kutumia mafuta ya samli kuhakikisha kuwa vinakaa jinsi
inavyotaakiwa,” anasema Mzee Lyakumba.
Anasema mwili wa marehemu huzikwa kwa kutazama
Mashariki kwa kuaamini kuwa, ndiko walikotokea Wahehe ‘kwetuhumile’
tulikotoka na katika baadhi ya koo ndani ya kabila hili, mfu hukalishwa
kwenye kiti anapozikwa.
Siku ya tatu baada ya maziko, ukoo
huhesabu idadi ya vyombo na nguo alizoacha marehemu na kupanga siku ya matanga
ambayo hutumika pia, kugawa vitu hivyo.
Mkubwa katika familia aliyoiacha marehemu
hupewa nafasi ya kwanza kuchukua kitu kimoja baada ya kingine anachokipenda.
Hufuatiwa na wadogo zake na baadhi ya watu kama mjomba, bibi, babu, kwa kufuata
taratibu za kimila.
Kwa upande wa ngoma, kabila hilo hucheza ‘kwa kufunga kengele na njuga ‘Mangala’ miguuni
huku wakicheza kwa kumzunguka mpiga
ngoma.
Aidha, ngoma hizo huchezwa wakati wa kufanya tambiko
pamoja na siku ya kugawa vyombo vya marehemu na endapo marehemu ameacha watoto,
familia ile huamini watatunzwa pasipo kushindwa ‘vana vakiva nunzaa
sivandema’ yaani watoto yatima nitawatunza hawatanishinda ni sehemu ya
wimbo anaoimbiwa marehemu aliyeacha watoto.
Kwa kufuata mila na desturi za Kabila hili, nafasi ya mwanamke awali alikuwa kama kichwa
cha familia ambapo alitegemewa na watoto kuwalipia ada na mambo mengine mengi
tofauti na sasa.
Katika enzi hizo
mwanamke alitakiwa kufanya kazi nyingi zaidi kuliko mwanamume.
Alijishughulisha
na mambo mbalimbali kikiwemo kilimo, kupika, kuokota kuni, kuchota maji,
kumbembeleza mtoto pamoja na kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kwa ajili
ya kuitunza familia.
Vile vile, si jambo la ajabu kwa mwanamke wa kabila
hili kutumiwa na mme wake kwa ajili ya kumtongezea mwanamke ambaye wakati
mwingine anaweza kuwa mke mwenza.
Asili ya nyumba za kabila hili ni za
udongo ambapo paa la nyumba huezekwa kwa
kutumia nyasi kavu tu, na nyingine
hutupiwa mchanga juu yake ili kuepuka kuunguzwa.
Ujenzi wa nyumba
hujengwa kulingana na familia iliyopo
kwa kuzingatia jinsia.
Kuhusu suala la mifugo, wanaume ndio wanaoipeleka
malishoni huku wakiwa wamebeba mkuki au mundu na fimbo.
Mvulana wa
kabila hili akifikia hatua ya
kubarehe huingizwa katika kundi la watu wazima kwani sasa anachukuliwa
kuwa anao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali hususan kilimo na katika ujenzi wa
nyumba.
Pia,
hufundishwa namna ya kuishi na watu mbalimbali katika mazingira tofauti.
Aidha, kijana huyo hupewa shamba lake ili
kumuandalia maisha ya kujitegemea.
Sambamba na hayo, msichana akipewa mimba
wakati bado yupo kwa wazazi na endapo
atakataa kumtaja aliyempa mimba, basi
huaminika kuwa amechafua nyumba ikiwa na maana kwamba mimba hiyo imetoka ndani
ya nyumba anayoishi.
Katika kumtia msukosuko zaidi familia
husika, ukifika wakati wa kujifungua
msichana huyo hutishiwa kuwa asipomtaja mwanaume aliyempa mimba atakufa.
Na kwa kuogopa kifo, hulazimika kumtaja
mhusika wa hiyo mimba.
Juu ya suala la uchumba, kabila hili
huzingatia mambo mbalimbali ikiwemo tabia
ya uchapaji kazi hususan kilimo na kuangalia kama ana uwezo wa kuimarisha
familia.
Posa ikishakubalika,upande wa mwanaumme
hutoa Jembe kama kitanguliza
Uchumba ‘Mkaja’ .
Mwanamke
anapopata mimba akiwa ndani ya ndoa baada
ya miezi saba tangu aolewe, mama yake anaenda kuomba ruhusa kule aliko
olewa ili akaishi naye hadi siku atakapo jifungua na baada ya kujifungua
hurudishwa kwa mumewe. Kuna mengi ya kujifunza katika kabila hili kwa ajili ya
faida ya kizazi kijacho.
No comments:
Post a Comment