MILA NA UTAMADUNI ZA KABILA LA WAHEHE KATIKA MKOA WA IRINGA
Iringa ni mji mkubwa uliopo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Ni makao makuu ya Mkoa wa Iringa na eneo lake ni Wilaya ya Iringa Mjini. Idadi ya wakazi ni takribani 112,000.
Asili ya jina la Iringa ni neno la Kihehe "liliga" lenye maana ya Boma. Mji umejengwa juu ya mlima ukitazama Mto Ruaha bondeni.
Mji wa Iringa upo kando la barabara kuu ya Tanzania - Zambia na kuna usafiri wa kila siku kwenda Dar es Salaam na Mbeya. Njia kwenda Dodoma ni sehemu ya barabara ya kale ya "Cape-Cairo" kati ya Rasi ya Afrika Kusini na Cairo ya Misri lakini kwa sasa ni barabara ya udongo tu.
Iringa ilianzishwa mwaka 1892 kama kambi la jeshi la kikoloni wakati wa vita ya Wajerumani dhidi ya Wahehe. Mji wa leo upo mahali pa "Neu Iringa" au Iringa mpya ya Wajerumani waliotumia jina hili baada ya kuharibu boma la mtemi Mkwawa huko Kalenga waliloita "Iringa" tar. 31 Oktoba 1894.
KABILA la Wahehe ambalo linapatikana mkoani Iringa, ni miongoni mwa makabila maarufu nchini ambalo halipo nyuma katika suala zima la kuenzi Mila na Tamaduni zake.
Wakati huo eneo ambalo sasa linaitwa Iringa lilikuwa na makabila mbalimbali. Walikuwepo ‘Wahafiwa’ katika Bonde la Milima Welu, Luvango, Wutinde, Lugulu, Makongati, Kalenga, Kipagala, Kihesa, Tambalang’ombe, Ibanagosi, Tipingi, Ikolofya, Nyambila, Kibebe na Isanzala.
‘Vanyategeta’ wao walioishi Udzungwa, Kitelewasi na Lundamatwe, ambao walikuwa wahunzi hodari. ‘Vanyakilwa’ walilowea Mufindi wakitokea Kilwa; ‘Vasavila’ waliishi milima ya Welu huko Makungu (Kihanga ya sasa), Magubike na Malangali; na ‘Vadongwe’ waliishi kando ya milima ya Uhambingeto, Ipogolo, Nyabula na Luhota.
Mbali na Kabila la Wahehe, Mkoa wa Iringa pia unakaliwa na Kabila la Wabena, Wapangwa, Wawanji na Wakinga. Japo sasa una mchanganyiko wa makabila mengine.
Kihehe ni lugha ya Kibantu nchini Tanzania inayozungumzwa na Wahehe. Hali kadhalika, Lugha ya Kihehe ya Kabila la Wahehe imegawanyika kutokana na Lahaja. Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia. Lahaja za lugha moja zatofautiana katika matamshi, miundo ya sarufi na msamiati. Kama lugha hutofautiana katika matamshi tu, tofauti hizo huitwa lafudhi na siyo lahaja. Uchambuzi na uchanganuzi wa lahaja ni tawi la isimujamii.
Wahehe wenyewe wanaweza kusikilizana bila tatizo lolote ila huweza kutambua ni mahali gani Mhehe huyu anatoka mfano Wahehe Vasungwa ambao wengi wao wanatoka eneo la Dabaga.
Suala la kuthamini tamaduni wanazorithi toka kizazi kimoja hadi kingine, ni moja ya sababu zilizowafanya Wahehe wajizolee sifa sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa sifa ambazo kabila hili limejizolea ni pamoja na uvumilivu, ujasiri, uchapaji kazi ambapo kwao kilimo cha mazao ya chakula ni msingi mkubwa wa maendeleo katika familia.
Anapobainika mtu mvivu, hudharauriwa na kuchekwa na ukoo mzima pamoja na jamii inayomzunguka.
Baadhi ya mazao yanayolimwa mkoani humo ni pamoja na mahindi, mtama, mihogo, alizeti, kunde, maharage, viazi vitamu, viazi mviringo, karangaa na ulezi.
Katika kilimo, kabila hili hufanya ushirikiano kwa namna ya kualikana baina ya mtu mmoja na mwingine na ushirikiano wa namna hii, hujitokeza wakati wa kupalilia na kuvuna.
Ukifika wakati wa mavuno, mtu anayesaidiwa kazi kwa siku hiyo huandaa pombe, togwa na kande kwa ajili ya wasaidizi wake. Kitendo hicho cha kualikana katika kazi huitwa ‘Mugove’.
Kulingana na mila za kabila hilo, hususan katika suala la kuandaa chakula, ni kwamba endapo mzazi mmoja atakuwa hayupo, mzazi anayekuwepo humsubiri mwenzake ili aungane naye katika mlo. Hii mara nyingi hufanyika kama kuna uhakika wa mzazi huyo kurudi mapema.
Hali ni tofauti kwa watoto kwani endapo mtoto wa kiume au wa kike atakuwa hayupo bila sababu maalumu, kimila haikubaliki hata kidogo kuwekewa chakula.
Chakula hicho ambacho huandaliwa na mwanamke au msichana hugawanywa katika makundi matatu. Mafungu haya ni pamoja na fungu la wazazi, wavulana na kundi la tatu ni watoto wa kike.
Katika kabila hilo, afikapo mgeni hushikana mkono wa kulia na mwenyeji wake na kila mmoja huanza kuubusu mkono wa mwezake kwa kupokezana mmoja baada ya mwingine zaidi ya mara tatu na kitendo hicho huitwa ‘Kinonela’/Kwinonela.
Mhehe katika kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo, mara nyingi hupenda kujisimamia mwenyewe ambapo huamini kuwa kusimamiwa ni kudhalilishwa au kudharauliwa.
Kabila hili pia, bado lina imani za kishirikina ambapo baadhi ya maeneo mkoani humo watoto wa vikongwe pamoja na ukoo wao huogopwa kwa namna moja au nyingine, hususan katika suala la kugombea mashamba likiwemo la wanafunzi.
Vile vile wanafunzi hushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao kwa kuhofia kufa. Siyo hivyo tu, hata kufanya shughuli za maendeleo mfano kujenga nyumba nzuri lilikuwa ni hatari sana siku nyuma, japo kwa sasa linapungua. Pengine mchanyiko wa makabila umepunguza imani hizi na kuchochea maendeleo.
Pamoja na kuwaogopa vikongwe miongoni mwa kabila hili huamini kuwa “Kufa konoga” wakimaanisha “kufa kupendeza” .
Usemi huu wa 'kufa kunoga' kwa Mhehe ni sehemu ya kujitia moyo na humuondolea hofu katika kukabiliana na matatizo mbalimbali ambapo kufa kwao ni jambo la kawaida kama ilivyopangwa na Mungu‘Nguluvi’.
Ugomvi mkubwa unaweza kutokea endapo mtu mmoja kutoka ukoo fulani atamnyooshea kidole mtu wa ukoo mwingine kwa lengo la kumkemea ‘Kufingulisa’/kufingula.
Kitendo hicho kikitokea yule aliyenyoshewa kidole huamini kuwa endapo atatokewa na baya lolote, litakuwa limetokana na yule aliyemnyooshea kidole.
Kabila hili la Wahehe, pia lipo mstari wa mbele katika suala la imani ambapo huomba baraka toka kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kutatuliwa matatizo mbalimbali na kuomba neema na msamaha.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa Mzee Albeto Lyakumba (63), kutoka Kijiji cha Lungemba mkoani humo, katika kabila hilo mtu anapokufa ndugu zake hawatakiwi kulia mapema mno, badala yake wanatakiwa kutulia kimya takribani saa moja baada ya kifo hicho./ Hufanya hivyo kwa lengo la kupata muda wa kutosha kuuweka vizuri mwili wa marehemu (maiti).
“Kitendo cha mtu kufa akiwa amekodoa macho au viungo vyake havijakaa sawia huwa tunakilaani sana, hivyo tunatumia muda huo kuuweka vizuri kwa kutumia mafuta ya samli kuhakikisha kuwa vinakaa jinsi inavyotaakiwa,” anasema Mzee Lyakumba.
Anasema mwili wa marehemu huzikwa kwa kutazama Mashariki kwa kuaamini kuwa, ndiko walikotokea Wahehe ‘kwetuhumile’ tulikotoka na katika baadhi ya koo ndani ya kabila hili, mfu hukalishwa kwenye kiti anapozikwa.
Siku ya tatu baada ya maziko, ukoo huhesabu idadi ya vyombo na nguo alizoacha marehemu na kupanga siku ya matanga ambayo hutumika pia, kugawa vitu hivyo.
Mkubwa katika familia aliyoiacha marehemu hupewa nafasi ya kwanza kuchukua kitu kimoja baada ya kingine anachokipenda. Hufuatiwa na wadogo zake na baadhi ya watu kama mjomba, bibi, babu, kwa kufuata taratibu za kimila.
Kwa upande wa ngoma, kabila hilo hucheza ‘kwa kufunga kengele na njuga ‘Mangala’ miguuni huku wakicheza kwa kumzunguka mpiga ngoma.
Aidha, ngoma hizo huchezwa wakati wa kufanya tambiko pamoja na siku ya kugawa vyombo vya marehemu na endapo marehemu ameacha watoto, familia ile huamini watatunzwa pasipo kushindwa ‘vana vakiva nunzaa sivandema’ yaani watoto yatima nitawatunza hawatanishinda ni sehemu ya wimbo anaoimbiwa marehemu aliyeacha watoto.
Kwa kufuata mila na desturi za Kabila hili, nafasi ya mwanamke awali alikuwa kama kichwa cha familia ambapo alitegemewa na watoto kuwalipia ada na mambo mengine mengi tofauti na sasa.
Katika enzi hizo mwanamke alitakiwa kufanya kazi nyingi zaidi kuliko mwanamume.
Alijishughulisha na mambo mbalimbali kikiwemo kilimo, kupika, kuokota kuni, kuchota maji, kumbembeleza mtoto pamoja na kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kuitunza familia.
Vile vile, si jambo la ajabu kwa mwanamke wa kabila hili kutumiwa na mme wake kwa ajili ya kumtongezea mwanamke ambaye wakati mwingine anaweza kuwa mke mwenza.
Asili ya nyumba za kabila hili ni za udongo ambapo paa la nyumba huezekwa kwa kutumia nyasi kavu tu, na nyingine hutupiwa mchanga juu yake ili kuepuka kuunguzwa.
Ujenzi wa nyumba hujengwa kulingana na familia iliyopo kwa kuzingatia jinsia.
Kuhusu suala la mifugo, wanaume ndio wanaoipeleka malishoni huku wakiwa wamebeba mkuki au mundu na fimbo.
Mvulana wa kabila hili akifikia hatua ya kubarehe huingizwa katika kundi la watu wazima kwani sasa anachukuliwa kuwa anao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali hususan kilimo na katika ujenzi wa nyumba.
Pia, hufundishwa namna ya kuishi na watu mbalimbali katika mazingira tofauti.
Aidha, kijana huyo hupewa shamba lake ili kumuandalia maisha ya kujitegemea.
Sambamba na hayo, msichana akipewa mimba wakati bado yupo kwa wazazi na endapo atakataa kumtaja aliyempa mimba, basi huaminika kuwa amechafua nyumba ikiwa na maana kwamba mimba hiyo imetoka ndani ya nyumba anayoishi.
Katika kumtia msukosuko zaidi familia husika, ukifika wakati wa kujifungua msichana huyo hutishiwa kuwa asipomtaja mwanaume aliyempa mimba atakufa.
Na kwa kuogopa kifo, hulazimika kumtaja mhusika wa hiyo mimba.
Juu ya suala la uchumba, kabila hili huzingatia mambo mbalimbali ikiwemo tabia ya uchapaji kazi hususan kilimo na kuangalia kama ana uwezo wa kuimarisha familia.
Posa ikishakubalika,upande wa mwanaumme hutoa Jembe kama kitanguliza Uchumba ‘Mkaja’ .
Mwanamke anapopata mimba akiwa ndani ya ndoa baada ya miezi saba tangu aolewe, mama yake anaenda kuomba ruhusa kule aliko olewa ili akaishi naye hadi siku atakapo jifungua na baada ya kujifungua hurudishwa kwa mumewe. Kuna mengi ya kujifunza katika kabila hili kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho.
No comments:
Post a Comment