Mtwara: Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza
Wananchi!
Na Zitto Kabwe - On Jan 20th 2013
Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana
na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa
na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo
kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara.
Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na
viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi
wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani
Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya
maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa
liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba, katiba ya nchi ibara ya 9 katika mabano J
inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli
zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri
au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza
kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara
wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za
kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa
Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa
Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa
wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu.
Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia
mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara
yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi
utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha
uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala
ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa
kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya
Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013
wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na
kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto
Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza
wananchi wanaodai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau
hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila
nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo
vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na
matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa
Mtwara ni kitendo kinachoweza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti
ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “Kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa
nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.” (Ibara ya 28, 1)
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina
ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata
kushirikisha Bunge. Inawezekana pia Serikali na hasa watendaji wa Serikali
waliojadili mkopo huu ‘wameshapata chao’ na hivyo kuogopa kusikiliza madai
halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu.
Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda
mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua
serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao.
Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa
Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara
alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate
majawabu!
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili.
Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na
kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani! Kwanini
Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja
mikataba mingine miwili, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya
dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za
kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila
kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi!
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya
fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba
imepandishwa maradufu. Wastani wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za
kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za
kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa
kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi
ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la
Mtera linalotegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12
ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi
itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya
kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama
wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya
magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo
tunayopendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania haki yao. Hii ni vita
ya uwajibikaji! Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa
vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye
rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa
kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.
No comments:
Post a Comment