MKANGANYIKO
NAMNA YA KUNUFAIKA NA RASLIMALI WALIGUBIKA TAIFA
§ Wazawa zinakotoka Raslimali hizo wanufaike kwanza, kisha baadaye
maeneo mengine
Taifa limekumbwa na mgawanyiko mkubwa
wa namna ya kunufaika na raslimali zinazopatikana hapa nchini. Uzoefu unaonesha
kuwa, watanzania wengi bado hawajanufaika kikamilifu na raslimali za asili
zinazopatikana kutoka katika maeneo yao. Maandamano yaliyofanywa na wananchi
kutoka Mkoa wa Mtwara, ni mfano tosha kuonesha kilio chao cha muda mrefu cha
kushindwa kunufaika na raslimali, hali ambayo wenye mamlaka na watunga sera
inabidi wajifunze.
Mkoa wa Mtwara, Lindi na Pwani imekuwa
ni maarufu kwa kilimo cha Korosho, zao la biashara ambalo limechangia kwa
kiwango kikubwa mapato ya kigeni. Korosho yenyewe haijawanufaisha kabisa wakazi
wa mikoa hiyo na hususani Mtwara ambayo ilikuwa bado iko nyuma kielimu,
kimiundombinu na kimaendeleo. Watunga sera na serikali kwa ujumla waliingilia
kwa kiasi kikubwa kupitia Bodi ya Korosho kusimamia soko na uuzaji wa zao la
Korosho. Matokeo ya udhibiti wa soko uliofanywa na serikali umeendelea
kuwadidimiza wakulima hao na pia kudidimiza zao la biashara la Korosho na hivyo
kuwasabishia machungu makubwa na umaskini.
Waswahili wana msemo huu, "Uking'atwa na Nyoka, hata ukiguswa na ujani
unashtuka". Wananchi wa Mtwara tayari wameng'atwa na nyoka kupitia zao
la biashara la Korosho. Kwa sasa hawana imani tena na watunga sera na
wasimamizi wa sera hizo. Wananchi hawa wana kilio cha kushindwa kunufaika na
zao la Korosho na matokeo yake kuendelea kuwa masikini.
Tofauti na ilivyotegemewa wengi, kuwa
kwa sababu zao la Korosho bado lipo kwenye soko tofauti na zao la Kahawa na Pamba
katika Mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Mwanza ambalo limekufa kabisa; ilibidi
hali yao ya kiuchumi iwe juu. Umasikini
ni somo kwao. Wamelitambua tatizo walilonalo na pia wamejitambua. Ndiyo maana
kwa sasa wameshikamana kuhusiana na mustakabali wa Gesi na Mafuta ambayo
yamegundulika katika pwani ya Mnazi Bay, katika Mkoa wa Mtwara.
Kwa nini wananchi hawa wanadai kuwa wa
kwanza kunufaika na raslimali hii? Hii inatokana na mifano mbalimbali ambayo
wanayo kutoka mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Arusha, Kagera na Mara ambapo mikoa
hii ilikuwa maarufu kwa uchimbaji wa Dhahabu, Almasi na Tanzanite. Je ni kwa
kiwango gani mikoa hii imenufaika na raslimali hizo?
Kwa upande wa Arusha huko Mererani
Wilaya ya Simanjiro ambayo ni mtoaji wa Tanzanite pekee duniani, bado kabisa
haijanufaika kikamilifu na raslimali hiyo. Wananchi wake bado ni maskini wa
kupindukia. Madini ya Tanzanite yanapoteza umiliki wake halali kiasi cha nchi
ya Kenya na Afrika Kusini kutawala soko la Tanzanite. Wananchi wa Mtwara
wameyaona haya na ndiyo maana waliandamana kudai kunufaika na Gesi.
Tanzanite imekuwa na mchango mdogo
sana katika pato la Taifa licha ya kuwa ni madini pekee duniani yanayopatikana
katika nchi ya Tanzania pekee. Hakuna usimamizi wa kina na mapato au bidhaa
zinazotokana na raslimali hii. Mwekezaji mgodini hapo yaani Tanzanite One
mkataba wake umeisha, lakini akapewa tena mkataba tata ambao wawakilishi wa
wananchi wamepiga kelele sana huko bungeni lakini hawakusikilizwa. Wananchi
wanaoishi kuzunguka katika migodi hii ni maskini wa kutupwa na wameangukia
katika lindi la migogoro isiyoisha na hata wakati mwingine kupoteza maisha yao.
Hili ni somo kwa wana Mtwara.
Mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Mara
ilijaliwa kuwa na raslimali ya Dhahabu na Almasi. Matokeo ya kuwepo kwa
raslimali hizo imesababisha mfarakano na vifo kwa wakazi wa mikoa hiyo. Kwa
mfano katika Mgodi wa North Mara, wananchi wengi wamepoteza maisha kutokana na
kuchafuliwa kwa mazingira na sumu, kuuawa na askari (kupigwa risasi) wakati
wanapoenda kuokota mabaki ya mawe yaitwayo Magwangwala ambayo wanafikiria
wakiyasaga wanaweza kupata kiasi kidogo cha madini ambayo wakiuza wanakidhi
mahitaji yao; kuachiwa mashimo yasiyo na kitu, kupoteza mifugo kutokana na
sumu; kuchafuliwa maji kutokana na kemikali zinazozagaa ovyo kwa sababu ya
kushindwa kudhibiti uharibifu wa mazingara na pia kuangukia katika wimbi la
umaskini. Wananchi hawa pia walizuiwa kushiriki katika uchimbaji mdogo mdogo wa
madini ambao ungewasaidia kupata kipato na kuweza kupunguza umaskini, kusomesha
watoto na pia kuzihudumia familia zao.
Kama ilivyo kwa mgodi wa North Mara,
huko Geita hali haikuwa tofauti kwa
sababu wananchi walihamishwa katika maeneo yao na kuachwa bila makazi. Baadhi
ya vijana walifukiwa mashimoni katika maeneo ambayo walikuwa wanachimba
dhahabu. Wachimbaji wadogo waliondolewa na kukosa kabisa eneo la kutafuta
riziki yao.
Kwa taarifa za sasa Ndugu Abrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM alitumia madaraka yake vibaya alipowapelekea wananchi
wanaoishi karibu na mgodi wa GGM leseni tano za uchimbaji mdogo, badala ya
shughuli hiyo kufanywa na wizara husika. Kitendo hiki kinatafsiriwa kuwa CCM
inawajali wakaazi hao kuliko wizara husika yenye dhamana hiyo.
Hali kama hii pia iliukumba mgodi wa Bulyahulu
ambapo kuna vijana wengi walifukiwa ndani ya migodi kwa kuelekezewa maji ya
mvua. Uhamishwaji usiofuata taratibu na ukatili wa kila aina ulifanyika kwao.
Matokeo yake wamebaki na wanaendelea kuwa masikini katika nchi yao yenye neema.
Katika mkoa wa Kagera, Mwanza na Mara
hali imendelea kuwa hivyo hivyo kama ilivyo mikoa mingine yenye raslimali. Kwa
mfano wakazi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wameendelea kukosa kabisa haki
ya kupata kitoweo cha samaki. Wameendelea kula mikia na vichwa maarufu kama
mapanki huku minofu ikisafirishwa nje ya nchi. Bei ya samaki ni kubwa mno kiasi
kwamba mwanachi maskini wa kawaida hawezi kumudu kumnunua samaki mmoja.
Wananchi wa mikoa hiyo walikuwa na
uvuvi wao wa asili huku wakilinda na kutunza mazingira ya ziwa hilo, lakini
wawekezaji walikuja na jina lao, wanaitwa wavuvi haramu. Humo ziwani kuna aina
nyingi ya samaki ambao wote waliliwa na Sangara aliyepandikizwa humo na kuua
vizazi vya samaki asili wa ziwa hilo; lakini serikali inasimamia Sangara tu
aina nyingine haitambuliwi kabisa. Ikumbukwe kuwa humo ziwani kuna aina ya
samaki ambao hata wakiwa na miaka kumi hawakui kufikia inchi mbili.
Hali kadhalika katika mgodi wa Almasi
huko Shinyanga hali ya umaskini kwa wakazi wanaoendelea kuzunguka machimbo hayo
ni kubwa na ya kutisha licha ya uchimbaji kuendelea kufanyika kwa takribani
miaka 32.
Wana Mtwara wasibezwe, waungwe mkono
kwa sababu wamejitambua na huu ndiyo wajibu wao. Kisingizio cha kusema kuwa
raslimali ziwanufaishe wananchi wote hii ni sawa lakini wenye nacho wapewe
kipaumbele, kwa sababu hata maendeleo baina ya mikoa yametofautiana na hii ni
sababu tosha.
Pamekuwepo na kujipendelea kwa baadhi
ya viongozi wanaopata fursa katika Baraza la Mawaziri kuelekeza uwingi wa
raslimali katika mikoa, wilaya na kata zao. Mfano pekee ambao ninaoukumbuka ni
kipindi ambapo Ndugu Basil Mrambo alipokuwa Waziri wa Fedha ambapoweza kutenga
kiasi cha shilingi bilioni 9 katika barabara ya hadhi ya kata, kipindi hicho
mikoa mingine ikishindwa kuunganishwa na barabara ya lami. Huu ni mfano mdogo
lakini kuna mifano mingi.
Wana Mtwara pengine wameangalia
asilimia ya fursa ambazo wamezipata wananchi kutoka katika mkoa huo katika vikao
vya kufanya maamuzi pamoja na kutunga sera. Kunyimwa kwa fursa hizo za kufanya
maamuzi pengine zimechangia kuifanya iendelee kuwa nyuma kimaendeleo.
Uamuzi wa sasa wa kung'ang'ania
kujenga bomba la gesi kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kuzalisha umeme si la
busara kabisa na ndiyo maana wakazi wa Mtwara wamelipinga. Kiasi cha Trilioni
Moja kilichobajetiwa kujenga bomba, ni vyema kingetumika kununua mitambo ya
kuzalisha umeme na kujengwa mkoani Mtwara. Hii itasaidia kuleta maendeleo
katika mkoa wa Mtwara huku ikitoa changamoto ya kuwa na Kiwanda Kikubwa (Big
Power Plant) ambazo itazalisha umeme ambao utaunganishwa kwenye gridi ya Taifa
toka huko huko Mtwara.
Pia siyo vyema na salama kila kitu
kujengwa Dar es Salaam maana yanaweza kutokea maafa kama vita au mafuriko ya
bahari ikizingatiwa kuwa Dar es Salaam ipo pembezoni mwa bahari. Ni vyema
tukawa na maeneo mengi ambayo yana mitambo ya umeme tukaepuka nchi kuwa gizani
kwa kuwa na chanzo kimoja kwenye umeme. Angalia hata viwanja vya ndege mbona
vimejengwa maeneo mengi nchini siyo tu Dar, hii inasaidia kukuza uchumi wa nchi
yetu.
Mwisho wa maoni yangu.
Imeandaliwa na:
Adam Kivenule
0713270364
kivenule@gmail.com
No comments:
Post a Comment