Tusipoandika historia yetu, tusije laumu ikipotoshwa!
By Michael
Dalali - On Jan 19th 2013
Wengi
wangependa kujua/kusoma wasifu rasmi “biography/autobiography” wa wanasiasa
kama Benjamin Mkapa, Dkt. Salim A. Salim (moja ya wanadiplomasia nguli ambaye
alipata kuiongoza Umoja wa Afrika katika miaka ya 1989 hadi 2001 kama Katibu
Mkuu na pia kuwahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Mwalimu Nyerere),
wafanyabiashara kama Said Salim Bakhressa, Reginald Mengi, wanazuoni kama
Profesa Issa Shivji, Haroub Othman. Wanamichezo kama Filbert Bayi, Leodgar
Tenga, n.k. ili kufahamu kwa undani wameweza kufika pale walipofika na kuwa na
mchango mkubwa mpaka sasa kwa taifa.
==================================================
Uandishi
umekuwa ukipungua siku hata siku katika jamii yetu ya Tanzania, lakini
haimaanishi hakuna vya kuandikwa, hakuna mafunzo ya kuwekwa katika kumbukumbu
kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo! Ni uchaguzi tu ambao wengi wenye
taarifa kuamua kutoandika historia ambapo madhara ya uamuzi huu ni makubwa
kuliko tabu ya kupitia mchakato wa uandishi.
Ni
kweli si kila mmoja ana karama ya uandishi lakini kwa ukuaji wa teknolojia na
maendeleo katika tasnia ya uandishi, hata asiye mwandishi anaweza kuandika iwe
yeye mwenyewe moja kwa moja au kushiriki katika uandishi pasi kuandika.
Tukiangalia
kwa haraka tunaweza kuhoji kwanini hakuna wasifu rasmi “biography/autobiography”
za kutosha za watendaji mbalimbali waliopata kushika ofisi za umma hasa ngazi
za juu na kutoa mchango mkubwa katika jamii yetu mpaka sasa. Lazima tujiulize,
kwani ni kwa kupitia maandiko kama hayo ndipo baadhi ya visa na mikasa ambayo
kwao wameipitia inaweza kuwa funzo maridhawa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwani ni thamani kuu kujifunza katika yale wengine walianguka au kuyamudu vyema
kuliko kusubiri yatukumbe tena ndipo tupate fundisho!
Ni
kwa namna gani, mathalani, majaji waliopata kutumikia mhimili wa mahakama kwa
muda mrefu na katika safari ndefu mfano wengine walioanzia toka uhakimu ngazi
za wilaya mpaka kufikia ngazi hizo za juu kabisa katika mhimili huo wa sheria
safari yao ikawa funzo na yenye kuhamasisha hasa kwa wanaoanza fani hiyo. Kwa
ukosefu wa maandiko kama hayo, wengi (hasa kizazi cha sasa) wanaweza hisi wanayoyapitia
ni mapya au kuyumbishwa na pia na misukumo mbalimbali. Kuna umuhimu mkubwa wa
maandiko haya.
Maandiko
haya pia hayapaswi kusubiri hadi muda wa kustaafu au uzeeni. Kuna machache
ambayo hata vijana wa sasa wameyapitia katika utendaji wao katika fani
mbalimbali ambayo yanaweza kabisa kuwa chachu kwa maendeleo na kupiga hatua
katika utendaji endapo yangeliandikwa vyema.
Katika
mjadala ambao nilipata kuuibua katika mtandao wa kijamii wa ‘Twitter’, wengi wa
wachangiaji walionyesha uhitaji sana wa kuandikwa kwa yale ambayo watu
wameyapitia au kukumbana nayo katika utumishi au utendaji kazi wao. Na baadhi
walidiriki kuonyesha kiu yao ya kutamani kusoma vitabu vyenye kuelezea misimamo
safari walizopitia katika taaluma nk baadhi ya watendaji wa kiserikali,
watumishi wa umma, wafanyabiashara, wanasiasa nk. Mifano michache ya kiu ya
wachangiaji ilikuwa ni kupata bahati ya kusoma wasifu rasmi “biography/autobiography”
wa wanasiasa kama Benjamin Mkapa, (aliyepata kuwa Rais wa Tanzania katika
serikali ya awamu ya tatu), Dkt. Salim A. Salim (moja ya wanadiplomasia nguli
ambaye alipata kuiongoza Umoja wa Afrika katika miaka ya 1989 hadi 2001 kama
Katibu Mkuu na pia kuwahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Mwalimu Nyerere),
wafanyabiashara kama Said Salim Bakhressa, Reginald Mengi, wanazuoni kama
Profesa Issa Shivji, Haroub Othman. Wanamichezo kama Filbert Bayi, Leodgar
Tenga, n.k. Haya ni kwa uchache tu, ambayo ni kiu kwa wengi kufahamu kwa undani
wameweza kufika pale walipofika na kuwa na mchango mkubwa mpaka sasa kwa taifa.
Ni kwa njia zipi, ipi ni misimamo yao katika baadhi ya masuala na nini ndoto
zao kwa Taifa letu.
Makundi
haya yanakwenda mbali pia kwa wale ambao bado wapo katika utumishi wao kwa
sasa, mathalani wanasiasa vijana kama; Zitto Kabwe, Halima Mdee, John Mnyika,
January Makamba ambao kwa hivi karibuni wamekuwa na mvuto na hamasa kwa vijana
wengi katika upande huo. Huku kusanifu pia maisha ya wajasiriamali vijana wenye
kumiliki makampuni na kuendesha biashara mathalani Mohammed Dewji. Lakini pia
wapo wenye kuhamasisha kutokana na mafanikio ambayo wamepiga katika taaluma na
kazi zao kama vile Suzan Mashibe kwenye shughuli za anga, Julie Makani katika sekta
ya afya. Ni muhimu kuandika historia sahihi ili isije ikaandikwa ndivyo sivyo!
Tumeshuhudia
uandishi kama huo ukifanywa kwa wanasiasa machachari wanaochipukia nchi
nyingine mfano Afrika Kusini ambako mwandishi Fiona Forde aliandika kitabu juu
ya mwanasiasa Julius Malema; “An Inconvenient Youth – Julius Malema and the
new ANC”.
Katika
kuhakikisha historia haipotei wala kufutika, kuna wengi walishiriki katika
ujenzi wa taifa na katika nyanja mbalimbali na kupitia utendaji wao hata kama
hawakuwa maarufu sana ila kuna maamuzi waliyopata kuyachukua yatadumu kuwa
funzo vizazi kwa vizazi. Bila ya kuwa makini na mafunzo haya tunakuwa jamii
inayorudia makosa yale yale kwa nyakati tofauti.
Tuchukulie
mfano katika eneo la usafirishaji wa majini ambalo katika miaka ya karibuni
tumeshuhudia ajali za kutisha zenye kuangamiza wananchi wengi. Lakini baadhi ya
matukio haya yamekuwa yakichangiwa na uzembe. Uzembe ambao miaka kadhaa nyuma
ulishakemewa na kwa nyakati zile ambazo tahadhari ilipuuzwa madhara
yalijitokeza. Hakuna uandishi wa vitabu wenye kutunza kumbukumbu hizi na
uchambuzi wa kina. Nyaraka nyingi za tume ambazo zinaundwa zinaishia kupata
vumbi katika makabati na kuliwa na mchwa. Lakini tungalichapa katika mifumo ya
vitabu na kufikika kwa wingi na mwananchi yeyote anayetaka kupata maarifa
kutokana nayo tungaliweza kupiga hatua.
Katika
kuzama kwa meli au vivuko tunaweza pia kukumbuka sakata mathalani la kuzama kwa
kivuko cha Kilombero. Kuzama huko kwa kivuko kulitokea kama ajali lakini
inaweza kuwa ni moja ya ajali ambazo ni tarajiwa kwani tayari uamuzi wa kununua
kivuko hicho ulipingwa vikali na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu
kwa wakati huo Marehemu Odira Ongara kwa madai kwamba kivuko kile kilikuwa
chakavu na kisingeweza kukidhi vigezo vya manunuzi na hata matumizi na kuamua
kutokutia sahihi ununuzi wa kivuko hicho. Uamuzi huu ulipuuzwa na kivuko
kikanunuliwa kwa uidhinishaji wa viongozi wengine wa juu zaidi, chini ya waziri
Mustapha Nyang’anyi na hatimaye maafa ya kuzama na kuua watu ndilo likawa zao.
Kuzama huko na maafa hayo vilizua mjadala mkali sana baadaye. Lakini kwa ufinyu
wa kuandika na kusoma, haya yamekuwa yakijirudia, makosa yaleyale yamezidi
kutusababishia maafa kwa taifa.
Mfano
wa eneo moja la sekta ya usafirishaji wa maji ni chembe tu katika mengi ambayo
yameshajitokeza kwenye sekta nyingine ambapo yamekuwa yakijirudia kila uchao
pasi kuwa na funzo kwa kizazi cha sasa wala kile kijacho.
Moja
ya hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu na ustawi wa taifa lolote ni pamoja
na kuthubutu kuandika na kusoma.
Jukumu
hili la kuweka kumbukumbu katika maandishi ni la kila mmoja ambaye amepitia
mengi ambayo yanaweza kuwa funzo kwa wengine iwe mazuri au mabaya awe ana uwezo
wa kiuandishi au lah, kwani kwa wale ambao hawana uwezo wa kiuandishi au muda
wa kuwekeza katika kuandika, wanaweza kabisa kushirikiana na wanahabari ambao
kwao uandishi ni sehemu ya kazi yenye kuwapatia kipato. Ndiyo inawezekana
kabisa, kwani katika nchi nyingi duniani, waandishi wa habari wamekuwa
wakitumia fursa ya kuwa karibu na vyanzo vya taarifa mbalimbali kuandika
maandiko kama vitabu aidha kwa niaba ya watu ambao wamepitia visa hivyo, au
wametenda masuala yenye kuhitaji kuwekwa katika kumbukumbu au pia kuandika tu
masuala nyeti kwa kina kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo.
Tunaweza
kujiuliza kwa kina kuna sababu gani kwa waandishi wa habari hususani wa makala
ambao kwa muda mrefu wameandika na kuchambua masuala ya rushwa katika sekta ya
nishati na madini yaani kusanifu mikataba mibovu ambayo imeingia katika historia
ya nchi yetu kama ile ya Richmond au Dowans kutokuwa na vitabu juu ya hayo? Ni
kwanini tunaruhusu haya yote ambayo tumeyashuhudia yapotee kwenye vichwa vyetu
pasi kuandikwa na kuwa funzo kwa vizazi vya sasa (hususan kwa nchi nyingine) na
vizazi vijavyo? Kuna sababu yoyote yenye tija katika hili? Au tutashangazwa
pale ambapo wataibuka waandishi toka nchi nyingine na kuandikia juu ya hayo
kisha tukahamasika na kukimbilia kuyasoma?
Kuna
nyakati zenye mafunzo mengi ya kisiasa ambayo endapo yakiachwa yapite pasi
kuandikwa vizuri tunaikatili historia yetu, tukichukua mfano mambo ambayo kundi
kama vile G55 ambalo lilikuwapo na kusimamia ajenda nyingi za kisiasa kama vile
suala la muungano na nafasi ya Tanganyika. Huko walikuwapo wanasiasa na wabunge
kama vile Njelu Kasaka, Jenerali Ulimwengu, hawa wote wapo. Mengi waliyopitia
ni tija sana katika hali ya kisiasa sasa na hata baadae. Ni funzo sana kwa
wanasiasa wa sasa na hata wa baadae. Tunahitaji sana maandiko yao!
Tunaweza
kujiuliza kwa wale ambao walipitia michakato ya kisiasa mathalani kushiriki kwa
kina na ukaribu chaguzi kama vile za mwaka 2005 na kushuhudia mikakati ya lile
kundi lisemwalo la “wanamtandao” wana sababu gani kutoandika mafunzo yale? Ni
woga? Au kwa wale ambao walishiriki kwa kina kampeni na michuano ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010 na hasa kampeni za upinzani za Dkt. Wilibrod Slaa ambaye
alikuwa moja ya mwanasiasa mwenye kugusa mioyo ya wananchi kutoandika tena kwa
kiuchambuzi juu ya yaliyojiri kwa kina? Ni woga?
Au
tunaweza kujiuliza: Kwanini hakuna uthubutu wa kuandika vitabu juu ya vyama
vyetu ambavyo vinaendesha siasa nchini mathalani vyama kama CHADEMA au CUF kwa
upande wa upinzani na kile chama tawala cha CCM? Kusanifu ukuaji wake,
kuimarika na hata misukosuko ambayo imeshapitia?
Maana
jamii yetu inapenda kusoma hayo, na ndiyo maana tunaona baadhi ya wananchi
wamekuwa wakinunua vitabu juu ya namna ambavyo siasa za Kenya zimekuwa
zikiendeshwa mathalani vitabu kama “Politics of Betrayal” (Siasa ya
Usaliti) cha Joe Khamis au kile cha “Peeling back the Mask” cha Miguna
Miguna. Hivyo ni miongoni mwa vitabu vya jirani wenzetu ambao wamekuwa
wakiandika yale ambayo wanapitia na kuwa funzo kwa sasa na baadae. Achilia
mbali nchi zilizoendelea kama vile Marekani ambako baadhi wamekuwa wakisoma
vitabu vingi juu ya namna siasa zimeendeshwa mathalani namna Rais wa sasa,
Barrack Obama amekuwa akiendesha kampeni zake na hatimaye ushindi katika vitabu
maarufu kama kile cha “Audacity to win” cha aliyekuwa meneja wa kampeni
za rais huyo Barrack Obama kwa mwaka 2008 bwana David Plouffe.
Hatuwezi
kupiga hatua kimaendeleo endapo hata masuala ambayo yapo katika uwezo wetu
hatuyatekelezi na kuyapa kipaumbele! Tunasaliti kuandika historia yetu wenyewe
hivyo ni fursa baadaye kwa kila yeyote yule anayeweza kunena juu ya hilo kuja
na kile anachopenda kisikike. Ukweli hasa wa mambo unapotea na kuachwa
upotoshaji uote mizizi!
No comments:
Post a Comment